Google yaipa Kenya Sh1.1 bilioni ijikwamue baada ya Covid-19 kusababisha uchumi kunywea

Google yaipa Kenya Sh1.1 bilioni ijikwamue baada ya Covid-19 kusababisha uchumi kunywea

Na CHARLES WASONGA na PSCU

KAMPUNI ya kiteknolojia ya Google imeipa Kenya Sh1.1 billioni (dola 10 milioni) za kupiga jeki juhudi za ufufuzi wa uchumi ulionywea kutokana na athari za janga la Covid-19.

Tangazo hilo lilitolewa Jumatano na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo ya asili ya Amerika, Sundar Pichai, wakati wa mkutano na Rais Uhuru Kenyatta kwa njia ya mtandao pembezoni mwa mkutano kuhusu maendeleo ya kidijitali barani Afrika.

Mkutano huo uliandaliwa na shirika la Corporate Council on Afrika (CCA) ambalo hujihusisha na mahusiano ya kibiashara kati ya Amerika na chumi za Afrika. CCA ina makao yake jijini Washington D.C.

Msaada huo wa kifedha unalenga kuzisaidia biashara ndogondogo na mipango mingine ya kusaidia jamii zisizo na uwezo.

“Zaidi ya hapo, kampuni yangu inalanga kusaidia biashara 100,000 na wabunifu 15,000 nchini Kenya mwaka huu, kifedha na kiteknolojia,”Bw Pichai akasema.

Katika sekta ya elimu, kampuni ya Google inalenga kutoa mafunzo kwa wanafunzi 29,000 na walimu 1,800 kwa kutumia programu yake maarufu kama “Google Classrooom platform.”

Rais Kenyatta alipongeza kampuni hiyo kwa msaada huo na kwa kujitolea kwake kupiga jeki juhudi za serikali za kuleta maendeleo ya kidijitali nchini ndani ya miaka 13 ambayo imeendesha shughuli zake Kenya

“Nakushukuru na kikosi chako kwa kuwa washirika wa karibu wa Kenya katika mawanda ya teknolojia kwa miaka mingi. Safari yetu ya kutumia teknolojia na mbinu za kidijitali katika kuendesha shughuli za serikali haswa katika sekta ya kifedha imeleta manufaa makubwa zaidi katika taifa letu. Biashara zetu pia zimenawiri; yote haya kupitia usaidizi wenu,” Rais Kenyatta akamwambia Bw Pichai.

Rais Kenyatta alisema Kenya imekuwa ikipanua uunganishwaji wa Intaneti kote nchini na kuwekeza katika mipango ya kuwawezesha vijana kunufaika kwa kupata ajira.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru, mwenzake wa masuala ya kigeni Rachel Omamo na Katibu katika Wizara ya ICT Jerome Ochieng’.

You can share this post!

BI TAIFA JANUARI 28, 2021

Minisketi zasababisha mvutano Malindi