Habari Mseto

#Google4Kenya: Huduma za Kiswahili, boda boda na Street View zazinduliwa

October 16th, 2018 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

KAMPUNI ya Google Jumatatu ilitangaza kuwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili sasa wana fursa ya kusaka taarifa mitandaoni kwa Kiswahili mufti huku ikizindua huduma mpya za kidijitali.

Kwenye hafla ya kampuni hiyo iliyoshirikisha Wizara ya Utalii mtaani Westlands, Nairobi, watumizi wa lugha ya Kiswahili waliagizwa kuanza kufurahia huduma ya kusakura habari kwa Kiswahili kama hatua moja ya kuimarisha utalii humu nchini.

Waziri wa Utalii Bw Najib Balala hata hivyo aliwataka wamiliki wa magari ya safari za utalii pamoja na wenye hoteli kuwawekea watalii huduma za intaneti almaarufu Wi-Fi ili kuwawezesha kusaka habari kwenye mitandao.

“Inasikitisha mno watalii kuambiwa na wenye magari na hoteli kuwa huduma za Wi-Fi zinakiuka haki za ubinafsi,” akasema Bw Balala na kuongeza kuwa Wizara yake tayari imeanza kutoa magari yenye huduma za intaneti kama mfano kwa wawekezaji katika sekta hiyo.

Aidha, Google ilitangaza kuwa Wakenya sasa wanaweza kununua programu za simu (apu) kutoka kwa duka la mtandaoni la Playstore na Appstore na kulipa wakitumia huduma ya M-Pesa.

Kampuni hiyo pia ilitoa msaada wa Sh100 milioni kutumia kuwafunza wakulima wa humu nchini kuhusu mbinu za kidijitali za kumarisha kilimo hasa katika uuzaji na ununuzi wa mazao.

Meneja wa Google Kenya Charles Murito alisema kuwa tayari kampuni hiyo imewapa mafunzo waundaji wa programu wapatao 9,000 huku jumla ya Wakenya milioni 2.5 pia wakifundishwa kuhusu mbinu za kisasa za biashara.

“Kati ya Wakenya 2.5 milioni, 625,000 wamekiri kushuhudia ongezeko la ukuaji wa biashara zao. Lengo letu ni kuhakikisha teknolojia zetu zimewasaidia watu wa matabaka yote,” akasema.

Bi Farzana Khubchandani ambaye ndiye meneja wa matangazo nchini Kenya, alielezea kuwa watumizi wa intaneti wa enzi za dijitali wanataka kupata majibu upesi zaidi.

“Ili kutimiza matakwa ya watumizi wa bidhaa zetu, tumeboresha huduma za Google Go na sasa tumezindua YouTube Go na Street View ili kuwapa Wakenya urojo wa teknolojia,” akasema.

Kampuni hiyo sasa imezindua huduma ya chaguo la bodaboda kwenye Google Maps kwa watu wanaotaka kusafiri hadi maeneo wasiyoyajua, na kuonyesha muda utakaotumika, ikilinganishwa na gari la kibinafsi, gari la umma na kutembea kwa miguu.

Bw Balala aliipongeza Google kwa kujitahidi kuweka huduma ya Street View kwenye mbuga za wanyama na maeneo ya vivutio ambapo watalii wataweza kusaka njia za mbugani.

“Mtu yeyote asiyetambua uvumbuzi na teknolojia ataangamia katika nyanja nyingi za maisha. Tunakoelekea utapata watalii wakihudumiwa na roboti hotelini. Lazima tubadilishe utalii wetu uwiane na maisha ya kisasa,” akasema.

Wizara ya Utalii ilisema itazidi kushirikiana na Google kwenye teknolojia zinazowafaa vijana kwani wengi watalii wanaouzuru maeneo mapya duniani ni vijana wa umri wa kati ya miaka 18 hadi 30.