Kimataifa

#GoogleWalkOut: Wafanyakazi wagoma kulalamikia dhuluma za kimapenzi ofisini

November 2nd, 2018 2 min read

MASHIRIKA NA PETER MBURU

WAFANYAKAZI wa Google Hong Kong na New York walitekeleza mgomo Alhamisi, wakilalamikia tabia ya unyanyasaji na dhuluma za kimapenzi ambazo walisema usimamizi wa kampuni hiyo ya kimataifa imekataa kuangazia.

Hii ilikuwa baada ya gazeti la New York Times kuchapisha habari kuwa kwa miaka sasa madai ya dhuluma za kimapenzi yamekuwa yakiendelea, maafisa wakuu kutochukuliwa hatua licha ya madai makali dhidi yao na ukosefu wa uwazi katika visa hivyo.

Wafanyakazi wa Tokyo hadi San Fransisco walihusika katika maandamano hayo, wakiondoka kutoka ofisi zao sa tano na dakika kumi za asubuhi, kuonyesha ghadhabu zao dhidi ya ripoti hizo.

Walitaja maandamano hayo ‘Google Walkout’, zaidi ya watu 1,000 wakiondoka kutoka ofisi za makao makuu ya Google eneo la Mountain View, California.

“Ni vibaya kuwa wanawake ambao wanavamiwa sharti wazungumze na watu walio na vyeo ili mabadiliko yafanyike,” akasema Taylor Reifurth, mhariri katika kampuni ya Google.

“Kwa kuwa wakati mwingine wanaowadhulumu ni wale ambao wako juu yao na ambao wako katika nafasi za kuwapandisha madaraka. Hivyo kusema ni kupoteza.”

Jiji la San Fransisco ambapo Google ina ofisi tano, zaidi ya wafanyakazi 1,000 wa kike na kiume waliungana wakiimba “haki za wanawake ni haki za wafanyakazi.”

Wengine walibeba mabango yaliyosuta pesa wanazopewa wanaodhulumu wafanyakazi ili wajiuzulu.

Wengi wa wafanyakazi walikiri kuwa wamewahu kudhulumiwa japo hawakuhudumiwa.

Bi Cathai Bi ambaye alizungumza kwa niaba ya wafanyakazi hao alisema wengi wao walikuwa na hofu ya kufutwa kazi kwa kushiriki mgomo huo, lakini wakaamua kuweka maslahi yao mbele.

Katika Jiji la New York, wafanyakazi walimiminika kutoka ofisi za makao makuu ya Chelsea na kujaza bustani iliyoko karibu wakiimba kuwa “muda umeisha” na kubeba mabango yaliyosema “haki za wanawake ni haki za binadamu.”

Maandamano hayo yalianzia Asia na kuendelea magharibi hadi Uropa na Marekani, takriban wafanyakazi 150 wa Google Asia wakishiriki maandamano hayo.

Google ina takriban wafanyakazi 2,000 miji ya Delhi, Mumbai, Bangalore na Hyderabad.

Katika ofisi za kampuni hiyo Singapore na Tokyo, kuliripotiwa visa vya wafanyakazi kuandamana vilevile na kuondoka kazini.

Kampuni ya Google pamoja za zingine za Silicon Valley na za kiteknolojia zimehusishwa na madai ya dhuluma za kimapenzi ofisini miaka ya majuzi na madai kuwa kuna tabia zinazotoa nafasi kw dhuluma za kijinsia na za ngozi wakati wa uajiri, kulipwa na kupandisha madaraka.

Waandalizi wa mgomo huo wa dunia waliandika katika gazeti la New York Times kuwa wanawataka viongozi wakuu wa kampuni hiyo kuchukua hatua mathubuti, zikiwemo kuondolewa kwa visa vya watu kulazimishwa kusamehe wanaowadhulumu.

Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa Google alisema kuwa aliunga mkono maandamano hayo na kususia kazi dhidi ya wafanyakazi, akisema “Tungetaka wateja wa google kufahamu kuwa tuna habari kuhusu maandamano yaliyopangwa Alhamisi na kuwa wafanyakazi watapewa msaada watakaohitaji wakati wa maandamano hayo,” alisema Jumatano.

“Tunapokea michango na mawazo ambayo wafanyakazi wamependekeza ili kuinua namna tunavyotoa huduma kutoka sasa,” akasema.

Lakini punde baada ya gazeti la Times kuchapisha ripoti hizo, usimamizi wa Google ulituma ujumbe ukisema kampuni hiyo imejitolea kuhakikisha kuwa mazingira ya wafanyakazi wake ni salama.

Gazeti hilo lilisema kuwa kampuni hiyo ilikuwa kimya kuhusu sakata hizo, na kuwakinga wakuu watatu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.