Gor, AFC Leopards waumiza nyasi bure alasiri nzima

Gor, AFC Leopards waumiza nyasi bure alasiri nzima

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Gor Mahia walidumisha rekodi yao ya kutoshindwa na mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards hadi mechi 10 kwenye Ligi Kuu baada ya kutoka 0-0 uwanjani Kasarani, Jumapili.

Pande zote zilijaribu kila mbinu kuonyeshana nani mbabe bila mafanikio uwanjani mtupu kwa sababu mashabiki hawakuruhusiwa ili kutekeleza masharti ya afya ya kuzuia janga la virusi vya corona ambalo limeua watu 1,776 humu nchini na visa 101,690 vya maambukizi kuripotiwa.

Gor, almaarufu K’Ogalo ilikuwa imebwaga Ingwe katika michuano sita mfululizo ya ligi kwa jumla ya mabao 14-3 kabla ya kupigwa breki katika gozi lao la Mashemeji ambalo lilikuwa la kusisimua.

Kwa kawaida, mashabiki wa timu hizo kongwe nchini humiminika katikati mwa jiji la Nairobi kuanzia mapema asubuhi, wakiimba na kucheza densi barabarani kabla ya kuelekea uwanjani.

Tofauti na makala yaliyopita, hawakuruhusiwa uwanjani, huku ulinzi mkali ukiwekwa Kasarani kutoka saa za asubuhi kuzuia mashabiki ambao wangejaribu kukiuka masharti hayo ya afya kutoka kwa serikali. Hata hivyo, mashabiki kadhaa walifanikiwa kutumia mabavu kuingia uwanjani.

Waliimbia na kucheza densi kwenye barabara za jiji kabla ya kulazimika kutafuta sehemu za burudani kutazama kwenye runinga mchuano huo mkubwa katika kalenda ya Kenya.

Kocha Carlos Manuel Vaz Pinto alikuwa ameonya vijana wake wa Gor dhidi ya kudharau Ingwe kutokana na kuwashinda mara sita mfululizo.

Walijituma kadri ya uwezo wao ikiwemo Jules Ulimwengu, Nicholas Kipkurui, Kenneth Muguna, Geoffrey Ochieng na Alpha Onyango kukosa lango pembamba ama kunyimwa na walinzi wa Ingwe, ingawa kipa Mganda Benjamin Ochan pia alikuwa macho michumani.

Ingwe ya kocha Anthony Kimani pia ilipata nafasi zake ikiwemo Harrison Mwendwa na Elvis Rupia kukosa lango. Kwa jumla, Rupia, ambaye anashikilia nafasi ya pili katika ufungaji nyuma ya Eric Kapaito wa Kariobangi Sharks, alibanwa na walinzi wa Gor.

Ingwe inasalia mbele ya Gor kwenye jedwali katika nafasi ya nne kwa alama 19 baada ya kusakata mechi tisa. Gor, ambayo inawakilisha Kenya kwenye Kombe la Mashirikisho la Afrika, ni ya sita kwa alama 16.

Katika mchuano mwingine uliochezwa jana, Bidco United ilizoa ushindi wa pili mfululizo kwa kuchabanga wenyeji Zoo 2-0 uwanjani Kericho Green.

You can share this post!

Raia waendeleza maandamano kupinga mapinduzi ya kijeshi

Morocco wapepeta Mali na kuhifadhi ubingwa wa taji la CHAN