Gor, AFC wajua wapinzani katika Betway 16-bora

Gor, AFC wajua wapinzani katika Betway 16-bora

Na GEOFFREY ANENE

GOR Mahia itavaana na Posta Rangers nayo AFC Leopards ilimane na Ushuru katika raundi ya 16-bora ya mashindano ya Betway FKF Cup, inayotarajiwa kuwa na msisimko wa aina yake mnamo Machi 14-15.

Timu zote 10 kutoka Ligi Kuu nchini (KPL) zilizoingia kipute hiki zilishinda mechi zao za raundi ya 32-bora, wikendi.

Washindi wa zamani Gor, Leopards, KCB, Sofapaka na Kariobangi Sharks pamoja na mabingwa watetezi Bandari na wanafainali wa 2016, Ulinzi Stars walijikatia tiketi.

Timu zingine kutoka KPL ambazo zilitinga awamu hiyo ya kuwania tiketi za kuingia robo-fainali ni Posta Rangers, Kisumu All Stars na Wazito.

Raundi hiyo ya 16-bora pia itashuhudia Talanta FC ikimenyana dhidi ya Kariobangi Sharks huku Sofapaka ikipimana ubabe na Bandari. Bidco United itakabiliana na Fortune Sacco, Vihiga United ikabane koo na Kisumu All Stars, KCB ifufue uhasama dhidi ya Wazito, nayo Migori Youth ipimwe makali yake na Ulinzi Stars.

Klabu tano kati ya 10 za KPL ziliingia raundi hiyo katika muda wa kawaida. Bandari ililipua KSG Ogopa 2-0, Sharks ilitoa dozi sawia kwa Kenpoly, Leopards ikang’aria Elim ya Kitale 1-0 nayo Wazito ikanyamazisha Egerton 1-0.

Gor pia ilifuzu katika dakika 90 baada ya kucharaza Naivas 3-2 japo kwa jasho, ilipolazimika kutoka nyuma mara mbili.

Rangers, Sofapaka, Kisumu All Stars, Ulinzi na KCB zilihitaji bahati pamoja na ujuzi wao wa ligi kubandua nje Tandaza, Balaji EPZ, Nyabururu Sportiff, Luanda Villa na Zoo Youth kupitia mikwaju ya penalti, mtawalia.

Fainali ya kombe hili ni Mei 30 ambapo mshindi atatia mfukoni Sh2 milioni. Aidha, atapata tiketi ya kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho Barani Afrika (Confederations Cup) msimu ujao.

Nambari mbili hadi nne watajiliwaza na tuzo ya Sh1 milioni, Sh750,000 na Sh500,000 mtawalia.

Ikiwa mshindi wa Betway Cup pia atanyakua ubingwa wa Ligi Kuu (KPL), basi timu itakayokuwa imefika fainali ya dimba hili itapata tiketi ya kushiriki Confederation Cup kama ilivyokuwa mwaka 2017.

Tusker ilishinda KPL na FKF Cup mwaka 2016 na hivyo kushiriki Klabu Bingwa Afrika 2017. Nayo Ulinzi iliyopoteza katika fainali ya kipute hicho ikaingia Kombe la Mashirikisho.

Jumapili, Gor ilisema kuwa itapigana kushinda mataji ya Ligi Kuu na pia Betway Cup msimu huu.

Imeshinda ligi kwa miaka mitatu mfululizo, lakini wako na ukame wa kombe hilo kwa miaka saba sasa.

“Tulitikiswa na Naivas lakini tumeng’amua mafunzo kadha. Mashindano yatazidi kuwa magumu lakini tutawania mataji yote nchini,” akasema naibu wa kocha, Patrick Odhiambo.

You can share this post!

Sportpesa watemwa EPL na klabu ya Everton

Matumaini ya Arsenal UEFA yangali finyu

adminleo