Michezo

Gor kuchuana na Kakamega Homeboyz 'tarehe nyingine'

April 10th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MECHI ya KPL ya Gor Mahia dhidi ya Kakamega Homeboyz imeahirishwa baada ya Gor kuendelea kushiriki katika mashindano ya CAF Confederation Cup.

Mechi hiyo iliyopangiwa kuchezwa Jumamosi Aprili 14 imeahirishwa hadi tarehe nyingine. Hii ni kulingana na ujumbe kwenye Twitter uliowekwa na kampuni ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

“Kutokana na ratiba ya timu ya Gor Mahia, mechi yake dhidi ya Kakamega Homeboyz iliyoratibiwa kuchezwa Aprili 14 imeahirishwa. Tarehe mpya itatolewa hivi karibuni.”

Vijana wa Dylan Kerr waliizima Super Sport United 1-0 katika raundi ya kwanza ya kufuzu kwa CAF Confederation Cup mechi ya makundi Aprili 8, na sasa ni zamu yao kusafiri jijini Pretoria, Afrika Kusini hapo Jumanne Aprili 17.

Kabla ya safari hiyo, Gor wataumiza nyasi dhidi ya Wazito FC ugani Machakos Aprili 11 katika mechi ya KPL. Ushindi dhidi ya Wazito utapunguza mwanya kati yao na Mathare United hadi pointi moja.