Michezo

Gor kumenyana na mahasidi wa Tunisia Klabu Bingwa Afrika

February 22nd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 16 wa Kenya, Gor Mahia, watafufua uhasama wao dhidi ya mabingwa mara 27 wa Tunisia, Esperance de Tunis hapo Machi 6, 2018 kwenye raundi ya kwanza (32-bora) ya Klabu Bingwa Afrika.

Gor walibandua nje Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kulazimisha sare ya 1-1 ugenini. Vijana wa kocha Dylan Kerr walishinda mechi ya mkondo wa kwanza 2-0 zaidi ya wiki moja iliyopita.

Esperance walijikatia tiketi ya kumenyana na Gor baada ya kulipua Concorde ya Mauritania kwa jumla ya mabao 6-1. Walitoka sare 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kuwika 5-0 Jumatano.

Gor na Esperance wamewahi kukutana katika mashindano haya ya kifahari mara nne katika Klabu Bingwa.

Gor waliibuka mabingwa wa Afrika mwaka 1987 kwa mabao ya ugenini baada ya kukaba Esperance 2-2 nchini Tunisia na kupata sare ya 1-1 nchini Kenya katika fainali.

Mwaka 2014, Gor walipepetwa 3-2 nchini Kenya kabla ya kunyeshewa mabao 5-0 katika mechi ya marudiano nchini Tunisia. Mechi hizi mbili zilikuwa za raundi ya kwanza.

Droo ya mechi za raundi ya 16-bora za Klabu Bingwa (2018):

Saint George (Ethiopia) vs. KCCA (Uganda)

Wydad Athletic Club (Morocco) vs. Williamsville AC (Ivory Coast)

Aduana (Ghana) vs. ES Setif (Algeria)

Al Ahly (Misri) vs. Mounana (Gabon)

MFM (Nigeria) vs. MC Alger (Algeria)

Horoya (Guinea) vs. Generation Foot (Senegal)

Young Africans (Tanzania) vs. Township Rollers (Botswana)

Gor Mahia (Kenya) vs. Esperance (Tunisia)

Etoile du Sahel (Tunisia) vs. Plateau United (Nigeria)

AS Togo (Togo) vs. El Hilal (Sudan)

Zesco (Zambia) vs. ASEC Mimosas (Ivory Coast)

TP Mazembe (DR Congo) vs. UD Songo (Msumbiji)

Difaa Hassan (Morocco) vs. AS Vita (DR Congo)

Primeiro de Agosto (Angola) vs. Bidvest (Afrika Kusini)

Rayon Sports (Rwanda) vs. Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

Armed Forces (Gambia)/Zanaco (Zambia) vs. Mbabane Swallows (Swaziland)