Michezo

Gor kumjua Jumatano mpinzani wao wa nane-bora katika CAF

March 19th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

GOR MAHIA iliweka hai matumaini ya kunyakua tuzo ya washindi ya Sh125.4 milioni baada ya kutinga robo-fainali ya soka ya Kombe la Mashirikisho la Afrika kwa kuchapa Petro de Luanda ya Angola 1-0 ikitumia wachezaji tisa mnamo Jumapili uwanjani Kasarani.

Mabingwa hawa wa Kenya, ambao mara ya mwisho walifika robo-fainali ya mashindano yoyote ya Afrika ilikuwa mwaka 1993, walirejea katika mduara wa nane-bora kupitia penalti ya mshambuliaji kutoka Rwanda, Jacques Tuyisenge.

Straika Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia asherehekea bao alilofunga dhidi ya Atletico Petroleos De Luanda katika mechi ya Kundi D iliyochezwa Machi 17, 2019, uwanjani Moi International Sports Centre, Kasarani. Picha/ Chris Omollo

Watafahamu wapinzani wao wa robo-fainali Machi 20 kutoka kwa orodha ya washindi wa makundi A, B na C ambao ni Berkane (Morocco), Sfaxien (Tunisia) na Al-Hilal (Sudan) mtawalia. Wakenya hawa hawawezi kukutanishwa na Hassania Agadir (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia) na Nkana (Zambia) katika robo-fainali kwa sababu pia walimaliza makundi yao katika nafasi za pili. Mechi za mkondo wa kwanza za robo-fainali ni Aprili 7, huku zile za marudiano zikisakatwa Aprili 14.

Baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Hussein Dey nchini Algeria na 4-0 dhidi ya Zamalek nchini Misri, Gor ilikuwa katika ulazima wa kushinda Petro ili kusonga mbele.

Iliingia mchuano huo wa mwisho wa Kundi D ikivuta mkia kwa alama sita, pointi mbili nyuma ya Zamalek na moja nyuma ya Petro na Hussein Dey.

Vijana wa Hassan Oktay hawakupata ushindi kwa urahisi.

Walistahimili mashambulizi makali na kumaliza mechi watu tisa. Walipata pigo la kwanza pale Ernest Wendo alilishwa kadi nyekundu dakika ya 36 alipokanyaga Vladmir Eston wa Petro kiunoni.

Mambo yalizidi kuwa mabaya Oktay alipoonyeshwa kadi nyekundu kabla tu ya mapumziko kwa kujibizana na wasimamizi wa mechi. Licha ya kuwa wachache pamoja na kumkosa Oktay kwenye kisanduku cha makocha, Gor ilirejea kipindi cha pili na kiu zaidi ya kupata ushindi.

Baada ya kubisha lango la Petro mara kadhaa, Gor ilipata penalti Bonface Omondi alipoangushwa ndani ya kisanduku pembeni kulia dakika ya 58.

Tuyisenge alifuma penalti hiyo kwa ustadi na kuimarisha rekodi yake ya kufungia Gor uwanjani Kasarani hadi mechi tano mfululizo.

Golikipa Peter Odhiambo alilazimika kufanya kazi ya ziada michumani dakika chache baadaye, huku Petro ikitafuta alama moja ambayo ingeitosha kuingia robo-fainali na kufungia Wakenya nje.

Odhiambo alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 68 kwa kupoteza wakati.

Sekunde chache baadaye, beki Harun Shakava pia aliingia katika kitabu cha refa kwa kulaani mchezaji wa Petro kujiangusha karibu na kisanduku.

Refa Mmoroko Redouane Jiyed kisha alionyesha Mganda Shafik Batambuze kadi ya pili ya njano katika mechi hiyo dakika ya 75 na kufanya Gor kusalia wachezaji tisa uwanjani.

Upungufu wa wachezaji wawili ulifanya Petro ijitume zaidi kupata bao. Hata hivyo, Gor ilikuwa imara kuondosha hatari.

Nusura la pili liingie

Lawrence Juma karibu aongeze bao la pili dakika ya 85 alipomegewa mpira mzuri na Tuyisenge, lakini shuti lake likagonga mlingoti na kutoka nje. Mabeki Shakava na Charles Momanyi karibu waitunuku Petro bao walipokosa kuwasiliana kila mmoja akiwachia mwenzake mpira.

Waligundua kosa lao haraka na kuondosha hatari Odhiambo akiwa ametoka michumani kuokoa timu yake.

Kocha wa Petro, Beto Bianchi pia hakumaliza mechi baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika muda wa ziada.

Kwa kufika robo-fainali, Gor tayari imejihakikishia tuzo ya Sh35 milioni.

Huenda ikatumia sehemu ya fedha hizi kugharamia utovu wa nidhamu wa mashabiki wa Gor kuingia uwanjani kusherehekea mara tu kipenga cha mwisho kulia.

Mwaka 2018 Gor ilivuna Sh27.5 milioni baada ya kampeni yake kufikia kikomo katika mechi za makundi za kipute hiki.