Gor kupiga mechi tatu kujiandalia Caf

Gor kupiga mechi tatu kujiandalia Caf

Na TITUS MAERO

VIGOGO wa soka nchini Gor Mahia wanaendelea kuimarisha maandalizi yao kwa mechi ya Kombe la Mashirikisho Afrika (Caf) wikendi ijayo, huku wakiratibiwa kushiriki mitanange ya kirafiki dhidi ya timu ngumu leo na wikendi katika Kaunti ya Kisumu.

K’Ogalo imepangiwa kuchuana na AS Otoho d’Oyo ya Jamuhuri ya Congo Novemba 28 ugenini kwenye raundi ya pili ya Caf huku ikiwa mwenyeji wa mkondo wa pili Disemba 5.Kwa mujibu wa kocha wa Gor Mark Harrison, mibabe hao watachuana na Muhoroni Youth leo katika uga wa Muhoroni Complex kabla ya kuvaana na Shabana na Kisumu All Stars mnamo Jumamosi na Jumapili.

Kwa kuwa ligi iliahirishwa kwa majuma mawili na kamati iliyochukua usukani baada ya kuvunjwa kwa Shirikisho la Soka Nchini (FKF), Gor inalenga kutumia mechi hizo kuhakikisha wachezaji wake wanasalia fiti kabla ya kuvaana na AS Otoho d’Oyo.’Ligi haiendelei na hatuwezi kutegemea maandalizi ya mazoezi pekee.

Hii ndiyo maana tunashiriki mechi hizi za kirafiki ili wachezaji wangu wawe fiti na pia kuimarisha mchezo wao kabla ya kipute cha Caf,’ Harrison akaeleza Taifa Leo.Mwenyekiti wa Muhoroni Youth Moses Adagala, mwenzake wa Kisumu All Stars Nicholas Ochieng na mkufunzi wa Shabana Robert Ojienda wote walithibitisha uwepo wa mechi hizo za kirafiki, wakisema pia timu zao zitanufaika.

‘Shabana ina historia pevu na Gor kutokana na uhasama uliokwepo tangu jadi. Tunachukulia mechi hii kwa uzito tukilenga ushindi na pia kuwa fiti kabla ya mechi za NSL kurejelewa,’ akasema Kocha wa Shabana Ojienda.

Timu itakayoshinda mechi hiyo ya raundi ya pili kati ya Gor na AS Otoho d’Oyo, itafuzu hatua ya makundi ambapo Caf hutoa Sh27 milioni kwa kila timu kusaidia katika kugharimia safari za michuano ya ugenini.

Gor ilifuzu mara ya mwisho kwa hatua ya makundi mnamo 2019, ilipolemea New Star ya Cameroon 3-1 katika raundi ya pili ya Kombe la Mashirikisho.Msimu huo Gor ilitinga robo fainali ila ikabanduliwa na RS Berkane kwa jumla ya 7-1.

You can share this post!

Hoki: Wakenya 2 kusimamia Klabu Bingwa Afrika

Simu 2 zilizotupwa na magaidi waliotoroka Kamiti zapatwa...

T L