Michezo

Gor kuvaana na Kariobangi huku Ingwe ikikabiliana na Ulinzi

February 22nd, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

 Ligi kuu ya KPL inarejelewa wikendi hii klabu za Gor Mahia  na AFC leopards zikishuka dimbani baada ya kushiriki mechi  za CAF, huku mashabiki wakiisubiri kwa hamu kuu.

Japo ligi hiyo inaingia kwenye raundi ya nne, Gor watakuwa wanacheza mechi yao ya tatu huku AFC leopards wakicheza mchuano wao wa pili.

Gor walifuzu kushiriki hatua ya pili ya kipute cha kuwania ubingwa wa Afrika baada ya kuwatandika Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa jumla ya mabao 3-1.

 AFC kwa upande wao waliondolewa kwenye kombe la Mashirikisho barani Afrika na Klabu ya Fosa Juniours kutoka kisiwa cha Madagascar kutokana na sheria ya CAF ya bao la ugenini.

Wana Ingwe walifungana 1-1 na timu hiyo uwanjani Bukhungu kisha wakatoka sare tasa kwenye mechi ya marudio.

Kwenye michuano ya ligi K’ogalo watakipiga dhidi ya kikosi cha Kariobangi Sharks uwanjani Machakos nao AFC wavaane na mabingwa wa zamani Ulinzi Stars uwanja wa manispaa waThika.

Kwenye msimamao wa ligi Gor wapo kwenye nafasi ya pili baada ya kushinda mechi zao mbili. Waliwachabanga Zoo Kericho 4-2 na Nakumatt FC 4-0.

Leopards wamecheza mechi moja tu dhidi ya Rangers walikotoka sare ya 1-1.

Mechi za KPL hata  hivyo zitaanza kugaragazwa Ijumaa hii kwa pambano kati ya vijana wa Francis Kimanzi Mathare united na Sofapaka yake Kocha Sam Ssimbwa.

Mathare United walikitia kibindsoni taji la KPL mara ya mwisho mwaka wa 2008 nao Ulinzi wakibeba ubingwa mwaka wa 2010.