Michezo

Gor Mahia katika mtihani mgumu wa kuhifadhi huduma za wanasoka tegemeo

June 10th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa Gor Mahia, Steven Polack ametaka usimamizi wa miamba hao kujitahidi kadri ya uwezo wao kuwadumisha kikosini wanasoka mahiri wenye ushawishi mkubwa zaidi uwanjani baada ya kubainika kwamba wengi wao wako pua na mdomo kuondoka.

Kati ya wanasoka matata ambao Gor Mahia wapo katika hatari ya kupoteza ni nahodha msaidizi Joash Onyango, beki Charles Momanyi na mshambuliaji Nicholas Kipkirui.

Siku chache zimepita tangu mwenyekiti Ambrose Rachier kukiri kwamba wachezaji wa Gor Mahia hawajalipwa mishahara kwa miezi mitano, tukio ambalo lilimfanya kudokeza uwezekano wa baadhi ya masogora wao kuwa wepesi wa kutafufa hifadhi kwingineko.

Huku akikiri kuwa hali si hali kambini mwa Gor Mahia, Polack sasa amewataka wasimamizi wa kikosi hicho kuwashawishi wanasoka wa haiba ambazo wamefichua azma ya kubanduka kutofanya hivyo.

Hilo, kwa mujibu wa Polack, litamwezesha kuyafikia mengi ya malengo yake katika soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) ambayo kikosi chake kitashiriki msimu ujao baada ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuwatawaza mabingwa wa muhula huu wa 2019-20.

Polack amesema kwamba anapania kusalia kambini na kikosi cha wanasoka 25 tegemeo ili kurahisisha shughuli ya kuwadhibiti, kutathmini maendeleo ya kila mmoja wao na hatimaye kusajili matokeo bora katika ulingo wa kimataifa.

Msimu jana, Gor Mahia walidenguliwa kwenye Kombe la Mashirikisho la Afrika (CAF Confederations Cup) baada ya kupokezwa kichapo cha jumla ya mabao 3-2 na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye mchujo wa makundi.

“Ili kujipa uhakika wa kuvuna matokeo ya kuridhisha katika soka ya CAF, italazimu kikosi kuhifadhi huduma za wachezaji mahiri kwa njia zote ziwezekanazo na kujishughulisha katika soko la usajili na kujinasia maarifa ya wanasoka wachache matata watakaoleta nguvu mpya na ushindani mkali,” akatanguliza.

“Mwaka jana, Gor Mahia hawakufanya vyema katika ulingo wa kimataifa baada ya kupoteza huduma za wachezaji wa haiba kwa mpigo. Hilo lilituweka katika ulazima wa kusajili wanasoka wengi kwa pupa na iliwachukua muda mrefu sana kuzoeana na kuoanisha mitindo yao ya usogora,” akasema Polack ambaye ni kocha wa zamani wa Asante Kotoko ya Ghana.

Kati ya wanasoka 25 ambao Polack anapania kusalia nao kikosini ni makipa watatu, mabeki wanane, viungo 10 na washambuliaji wanne.

Japo ameshikilia kwamba alianza kujiandaa kwa kampeni za msimu ujao yapata majuma matano yaliyopita, Polack amefichua uwezekano wa kuagana na Gor Mahia iwapo huduma zake zitawaniwa na kikosi kinachojivunia uthabiti zaidi wa kifedha ndani au nje ya bara la Afrika.