Michezo

Gor Mahia kuchafuana leo na Western Stima mjini Kisumu

February 12th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

GOR Mahia wanatarajiwa leo Jumatano kujinyanyua dhidi ya Western Stima katika mchuano wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), utakaowakutanisha na Western Stima uwanjani Moi, Kisumu na kuweka hai matumaini ya kutawazwa mabingwa kwa mara ya 19.

Miamba hao wa soka ya humu nchini watajibwaga ugani siku tatu baada ya kupokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Sofapaka ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane kwa alama 30 chini ya kocha John Baraza ambaye ni mvamizi wa zamani wa Harambee Stars.

Mchuano wa wikendi jana ulikuwa wa tatu kwa Gor Mahia kupoteza hadi kufikia sasa muhula huu. Gor Mahia wana ulazima wa kusajili ushindi hii leo ili kuepuka presha kutoka kwa Tusker na Kakamega Homeboyz ambao ni miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la KPL muhula huu.

Kufikia sasa, Gor Mahia wanaselelea kileleni mwa jedwali la KPL kwa alama 44 huku pengo la pointi tatu pekee likitamalaki kati yao na Tusker ambao ni mabingwa mara 11.

Kupaa kwa Tusker ambao kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya 13 zilizopita chini ya kocha Robert Matano, kulichochewa na ushindi wa 1-0 waliousajili dhidi ya mabingwa mara 13 AFC Leopards katika kipute kilichowakutanisha ugani Afraha, Nakuru wikendi jana. Bao hilo la pekee lilifumwa wavuni na mvamizi Timothy Otieno ambaye kwa sasa anajivunia jumla ya magoli 11 kapuni mwake.

Chini ya mkufunzi Nicholas Muyoti, Homeboyz ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko wapinzani wao hawa wakuu, wanafunga mduara wa tatu-bora kwa alama 41 baada ya kupiga jumla ya mechi 20 ambazo zimewashuhudia wakiambulia sare mara tano na kuzidiwa maarifa mara tatu.

Ingawa hivyo, Homeboyz huenda wakarushwa hadi nafasi ya nne iwapo wanabenki wa KCB watawapepeta Bandari FC ugani Mbaraki Sports Club katika mchuano mwingine wa leo Jumatano wa KPL.

KCB ya kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno kwa sasa inashikilia nafasi ya nne kwa alama 38, mbili zaidi mbele ya Ulinzi Stars ambao wanajivunia kutawazwa wafalme mara nne.

Chombo cha wanabenki hao kilizamishwa kwa 1-0 na Kariobangi Sharks mwishoni mwa wiki iliyopita huku Ulinzi Stars wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Nzoia Sugar.

Bandari wanakamata nafasi ya 11 kwa alama 20 na pengo kubwa la alama tisa linatamalaki kati yao na Posta Rangers na Mathare United wanaofunga orodha ya tisa-bora.

Washindi hao wa zamani wa Shield Cup wana ulazima wa kutia kapuni alama zote tatu mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ili kuepuka hatari ya kushuka zaidi na kuingia katika orodha ya vikosi vitakavyoteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu.

Bandari watajibwaga ugani wakitawaliwa pia na kiu ya kusajili ushindi baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Homeboyz wikendi iliyopita jijini Mombasa.

RATIBA YA KPL (Leo Jumatano)

Bandari na KCB (Saa Nane, Mombasa), Western Stima na Gor Mahia (Saa Tisa, Kisumu).