Gor Mahia na Ingwe zavuna pakubwa kwa kupata mdhamini mpya

Gor Mahia na Ingwe zavuna pakubwa kwa kupata mdhamini mpya

Na CECIL ODONGO

WIKI tatu tu baada ya Betsafe kujiondoa kama wadhamini wa Gor Mahia na AFC Leopards, timu hizo jana zilivuna nafuu baada ya kupata mdhamini mpya hata kabla ya msimu ujao kuanza.

Gor na AFC ambazo zimeshinda kwa jumla mataji 32 ya Ligi Kuu (KPL), zitafadhiliwa kwa kima cha Sh70 milioni na Sh60 milioni mtawalia na kampuni ya kamari Spotika kwa muda wa miaka mitatu. Hii ni mara ya kwanza ambapo kampuni hiyo inaendeleza biashara yake hapa nchini.

Kwa mujibu wa Katibu wa Gor Mahia Sam Ochola, pande zote zinatarajiwa kumwaga wino kwenye kandarasi hiyo ambayo itahakikisha Gor inapata Sh7 milioni kila mwezi. Pia kuna manufaa mengine kwenye dili hiyo ambapo Spotika itawapa wachezaji jezi na viatu vya kuchezea.

“Ndiyo tumepata mfadhili mwengine na ni kampuni ambayo inaingia katika soko la Kenya kwa mara ya kwanza. Hizi ni pesa ambazo zitatusaidia sana katika kuwalipa wachezaji mishahara na pia kutimiza maslahi mengine ndani ya klabu,” akasema Ochola.

Aidha hafla rasmi ya kuzindua ufadhili huo kwa upande wa AFC Leopards utafanyika leo katika hoteli moja jijini Nairobi kisha ya Gor baadaye. Ufadhili huo unakuja siku chache tu baada ya timu hizo mbili kufika katika ikulu na kutuzwa Sh4 milioni alizoahidi Rais Uhuru Kenyatta mnamo Mei 8 wakati wa debi ya Mashemeji katika ikulu ya Nairobi.

Gor na AFC Leopards zimekuwa zikipata wafadhili ila mara nyingi huwa kampuni hizo hazimalizi kandarasi yao. Betsafe ilitia saini kandarasi ya miaka mitatu na Betsafe mnamo 2020 ambapo Gor na AFC zilikuwa zikipata Sh 55 milioni na Sh40 milioni mtawalia kila msimu.

Hata hivyo, pesa hizo zilipunguzwa hadi nusu kwa timu zote mbili kutokana na athari ya virusi vya corona. Betsafe pia ilikuwa ikiwatuza wachezaji wa timu zote mbili waliong’aa kila mwezi Sh25,000.

Vilevile, Gor na AFC Leopards zilikuwa zikinufaika na ufadhili wa Sportpesa kwa kima cha Sh198 milioni na Sh156 milioni mtawalia kwenye mkataba wa miaka mitatu uliotiwa saini mnamo 2018.

Hata hivyo, mkataba huo uliofaa kukamilika 2021 haukukamilika baada ya SportPesa kujiondoa kutokana na ushuru wa juu uliokuwa ukitozwa kampuni za kamari na serikali.

Kati ya 2011 hadi 2014 wakati ambapo AFC Leopards walikuwa wakidhaminiwa na kiwanda cha sukari cha Mumias, Gor Mahia nao walikuwa wakifadhiliwa na kampuni ya maziwa ya Tuzo kwa kima cha Sh38 milioni katika miaka miwili ya mwanzo kisha ikaongeza Sh29 milioni nyingine kabla ya kandarasi hiyo kutamatika 2014.

  • Tags

You can share this post!

Nabirye ateuliwa kikosi cha Uganda michuano ya AWCON

Hakuna ufadhili kwa mashirikisho ya michezo, wizara yasema...

T L