Michezo

Gor Mahia wajinolea ligi baada ya fedheha CAF

October 1st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia walirejelea mazoezi Jumatatu baada ya kubanduliwa nje ya soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF).

Vijana wa kocha Steven Polack walifika uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi na kufanya mazoezi baada ya timu yao ya chipukizi, Gor Mahia Youth, na timu ya taifa ya wanawake Harambee Starlets kutumia uwanja huo.

Gor, ambayo ilichapwa 2-0 na USM Alger ya Algeria katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani katika mechi ya raundi ya kwanza ya marudiano na kuaga mashindano hayo ya daraja ya juu kwa jumla ya mabao 6-1, imeratibiwa kulimana na Nzoia Sugar hapo Jumatano kwenye Ligi Kuu.

Itakuwa ikitafuta ushindi wake wa nne mfululizo katika ardhi yake dhidi ya wanasukari hao na pia kulipiza kisasi baada ya kulemewa 1-0 ugenini timu hizi zilipokutana mara ya mwisho mnamo Mei 15.

Kuvuna alama

Gor almaarufu K’Ogalo inashikilia nafasi ya nane kwa alama sita ilizopata kwa kutitiga mabingwa wa zamani Tusker 5-2 na wanabenki wa KCB 2-1.

Vijana wa Polack wataruka juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 18 wakivuna alama tatu dhidi ya Nzoia.

Kwa sasa, wanaumeme wa Western Stima wako juu kwa alama nane kutokana na ushindi mara mbili na sare mbili.

Baada ya kupigwa na USM Alger, Gor sasa itashiriki Kombe la Mashirikisho la Afrika.