Michezo

Gor Mahia yaanza kunusa taji la ligi

November 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Gor Mahia wako katika orodha ya klabu nane zilizopiga hatua kubwa kwenye jedwali la ligi kuu baada ya mechi za raundi ya tisa Jumapili.

Gor ya kocha Steven Polack, ambayo ilikuwa imepata pigo katikati ya juma lililopita iliponyukwa 1-0 na washindi wa mwaka 2008 Mathare United, sasa inaongoza ligi hii ya klabu 18 kwa alama 18 kutokana na mechi saba.

Imeingia likizo ya mechi za mataifa ikifurahia kuwa na mechi mbili mkononi dhidi ya wapinzani wa karibu Kakamega Homeboyz, mabingwa wa zamani Tusker na Mathare wanaofuatana katika nafasi za pili, tatu na nne kwa alama 17 kila mmoja. Homeboyz ilirukia nafasi ya pili kutoka nambari tano baada ya kunyamazisha majirani Western Stima 2-0.

Tusker, ambayo ilikuwa kileleni kabla ya mechi za raundi ya tisa, imerushwa chini nafasi mbili. Inashikilia nafasi ya tatu baada ya kutolewa kijasho chembamba na KCB katika sare ya 1-1 Jumamosi.

Mathare ndiyo timu pekee iliyoshinda ugenini wikendi iliyopita. Ilichapa washindi wa mwaka 2006 SoNy Sugar 3-2 uwanjani Awendo na kutulia katika nafasi ya nne baada ya kupaa nafasi mbili.

Mabingwa wa zamani Ulinzi Stars wanashikilia nafasi ya tano baada ya kujinyanyua kutoka nambari nane walipozamisha Bandari bao 1-0 ugani Afraha.

Wanajeshi wa Ulinzi wamezoa alama 16. Wako alama moja mbele ya nambari sita KCB, ambao wamesakata mechi moja chache. Wanabenki wa KCB waliteremka nafasi mbili baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na Tusker katika mechi iliyoshuhudia beki wa KCB, Bethuel Warambo akionyeshwa kadi nyekundu baada ya kuchezea Michael Madoya visivyo.

AFC Leopards ndio waliopiga hatua nyingi nyuma. Baada ya kuaibishwa 4-1 na Gor, vijana wa kocha Casa Mbungo waliporomoka kutoka nafasi ya tatu hadi nambari saba. Ingwe imezoa alama 15, lakini inazidiwa na KCB kwa tofauti ya magoli.

Posta Rangers imeruka juu nafasi moja hadi nambari nane baada ya kulipua Chemelil Sugar 3-0. Rangers ina jumla ya alama 14. Inafuatwa na Stima, ambayo imevuna alama 13 kutokana na mechi nane.

Stima, itakayomenyana na Tusker katika mechi ijayo, iko chini nafasi mbili japo haijasakata mechi moja.

Mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka wanafunga mduara wa 10-bora baada ya kuimarika kutoka nafasi ya 12.

‘Batoto ba Mungu’ walilemea mabwanyenye Wazito 2-1 na kufikisha alama 11.

Bandari na Wazito wako chini nafasi moja katika nafasi ya 11 na 12 kwa alama 11 na 10, mtawalia. Bandari, ambayo itaalika Leopards katika mechi yake ijayo, ina mechi moja mkononi.

Zoo ilibwaga Nzoia Sugar 2-1 na kuruka wanasukari hao. Klabu hiyo kutoka kaunti ya Kericho ni ya 13 kwa alama 10. Nzoia iko chini nafasi moja katika nafasi ya 14. Imezoa alama nane, moja zaidi ya Kariobangi Sharks, inayokamilisha orodha ya timu zilizo nje ya mduara hatari wa kutemwa.

Kisumu All Stars iliyozoa ushindi wake wa kwanza, ilipochapa Sharks 1-0 uwanjani Moi, Jumamosi. Ushindi huo ulisaidia Kisumu kurukia nafasi ya 16 kwa alama sita. SoNy ni ya 17 kwa alama nne baada ya kushuka nafasi moja.

Chemelil, klabu pekee ambayo haijapata ushindi msimu huu, inavuta mkia kwa alama moja.