Gor Mahia yapigiwa chapuo kuendeleza ubabe kwenye kampeni za ligi kuu

Gor Mahia yapigiwa chapuo kuendeleza ubabe kwenye kampeni za ligi kuu

Na JOHN KIMWERE

MIAMBA wa soka nchini, Gor Mahia wikendi hii watashuka dimbani kukabili Sofapaka FC kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Betking Kenya Premier League (BKPL) kuwinda pointi tatu muhimu.

Gor Mahia itaingia dimbani katika uwanja wa Thika, Jumamosi kutifua vumbi dhidi ya Sofapaka FC iliyolazimishwa na Ingwe kutoka nguvu sawa mabao 2-2.

K’Ogalo ya kocha, Carlos Manuel Vaz Pinto inazidi kupiga hatua kimzaha katika msimamo wa kipute hicho licha ya kusajili ushindi mwepesi dhidi ya wapinzani wao.

Tangu michezo kurejelewa, Gor Mahia imeonekana inazidi kufufua kampeni zake ambapo imeshinda mechi sita mfululizo.

K’Ogalo imefanikiwa kusajili ushindi wa alama tatu kwa kila moja dhidi ya Bidco United, Nairobi City Stars, Sofapaka FC, Vihiga United, Wazito FC na Mathare United.

Matokeo ya K’Ogalo kwenye mechi za hivi karibuni yameanza kuiweka pazuri kwenye kampeni za kutetea taji hilo. Hata hivyo yanazitia njeve klabu zingine ikiwamo KCB, AFC Leopards bila kuweka katika kaburi la sahau Tusker FC.

Katika jedwali la kipute hicho, KCB ambayo itaingia mzigoni kucheza na Mathare United inaongoza kwa kuzoa alama 39, moja mbele ya Tusker.

You can share this post!

Uholanzi wacharaza Austria na kuingia 16-bora kwenye...

Mutua akubali Ruto ni maarufu Mlima Kenya