Michezo

Gor Mahia yasema iko tayari kwa mtihani wa APR katika gozi la CAF Champions League

November 12th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

GOR Mahia watakuwa wageni wa Armee Patriotique Rwandaise Football Club (APR) ya Rwanda mnamo Novemba 28 kwenye mkondo wa kwanza wa mchujo wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) mnamo 2020-21.

Kwa mujibu wa droo hiyo iliyofanyika jijini Cairo, Misri, Gor Mahia watakuwa wenyeji wa gozi la marudiano litakalotandazwa kati ya Disemba 4-6. Mechi hizo zitawakutanisha Gor Mahia na fowadi wao wa zamani, Jacques Tuyisenge aliyesajiliwa na APR mnamo Septemba kutoka Petro de Luanda ya Angola.

Hadi alipoyoyomea Angola mnamo Agosti 2019, Tuyisenge alikuwa amevalia jezi za Gor Mahia kwa misimu mitatu na kuongoza mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya na washindi mara 19 kutwaa mataji matatu ya kivumbi hicho.

Kocha mpya wa Gor Mahia, Roberto Oliveira Goncalves kutoka Brazil, atapata pia fursa ya kuchuana upya na APR ambao ni watani wa tangu jadi wa waliokuwa waajiri wake, Rayon Sport waliowahi kuvaana na Gor Mahia kwenye hatua ya makunzi ya Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) mnamo 2018.

Mshindi wa michuano ya mikondo miwili kati ya Gor Mahia na APR atakutana ama na El Nasr ya Libya au mabingwa wa Algeria, CR Belouizdad.

Gor Mahia walichuana na APR kwa mara ya mwisho mnamo 2014 kwenye hatua ya makundi ya kipute cha Cecafa Kagame Cup na kuambulia sare ya 2-2 nchini Rwanda.

Alipoajiriwa na Gor Mahia ambao hawajawahi kufuzu kwa hatua ya makundi ya CAF Champions League, kocha Oliveira alisema kwamba lengo lake ni kuongoza miamba hao kutinga hatua hiyo na kuingia mduara wa nane-bora.

“Ingawa kuanza ugenini ni afueni tele, kibarua kilichopo mbele si rahisi. Kila timu inayofuzu kwa mashindano haya ni mpinzani asiyestahili kubezwa,” akasema kocha msaidizi wa Gor Mahia, Patrick Odhiambo.

“Tuko tayari kwa mtihani wa APR. Kinachotuaminisha zaidi ni umahiri wa wachezaji tuliowasajili hivi karibuni,” akaongeza Odhiambo kuwa kusisitiza kwamba wanalenga kuimarisha zaidi maandalizi yao kwa minajili ya kibarua cha CAF na mashindano ya Ligi kuu.

Gor Mahia ambao waliagana na wanasoka 15 watapania kutegemea pakubwa huduma za sajili wapya 16 waliojiunga nao muhula huu kwa minajili ya kampeni hizo za CAF. Gor Mahia watavaana na APR wiki moja baada ya kushuka dimbani kumenyana na wafalme mara 11 wa taji la KPL, Tusker FC mnamo Novemba 21 kwenye mechi ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya FKFPL.

Katika kampeni za msimu jana, Gor Mahia walibanduliwa mapema kwenye hatua ya mchujo wa CAF Champions League baada ya kupokezwa kichapo cha jumla ya mabao 6-1 na USM Alger ya Algeria. Kubanduliwa kwao kuliwashusha ngazi hadi CAF Confederation Cup ambao walidenguliwa na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa magoli 3-2.

Gor Mahia walinyanyua taji la kimataifa la Afrika mnamo 1987 walipocharaza Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia na kutwaa ubingwa wa Mandela Cup. Walitinga robo-fainali za Caf Confederation Cup kwa mara ya kwanza mnamo 2018.

Kenya haitakuwa na mwakilishi wa moja kwa moja kwenye CAF Confederation Cup msimu huu baada ya janga la corona kusababisha Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kushindwa kutamatisha kampeni za FKF Shield Cup ambazo humpa mshindi fursa ya kunogesha kipute hicho.

Simba SC ya Tanzania inayojivunia huduma za Wakenya Francis Kahata na Joash Onyango wamepangwa kukutana na Plateau United ya Nigeria kwenye CAF Champions League huku Nkana FC inayowapa hifadhi Wakenya Harun Shakava na Duke Abuya wakikutanishwa na Bantu FC ya Lesotho. Raja Club Athletic na Wydad Club Athletic kutoka Morocco hawatashiriki mechi za raundi ya kwanza za CAF Champions League kwa pamoja na Al Ahly ya Misri na Horoya ya Guinea baada ya kutinga hatua ya nusu-fainali msimu uliopita.

Vikosi vingine vitakavyoepushwa kunogesha hatua hiyo ni Esperance, Zamalek SC, TP Mazembe, Mamelodi Sundowns, AS Vita Club na Primero de Agosto ya Angola.