Gor Mahia yawasaka wavamizi 3 nje ya nchi

Gor Mahia yawasaka wavamizi 3 nje ya nchi

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Gor Mahia imetangaza kuwa inawasaka washambulizi watatu hatari zaidi kutoka nje baada ya kuwatema Tito Okello na Jules Ulimwengu.

Mkufunzi wa Gor Mahia Mark Harrisson, Alhamisi alieleleza Taifa Leo kuwa timu hiyo ipo pua na mdomo kuwanasa washambulizi wembe kutoka Nigeria, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Tito na Jules wameondoka klabuni na sasa tumetambua washambulizi wawili ambao nimependekeza wasajiliwe. Tayari mchakato huo unaendelea na watawasili hapa nchini tukianza maandalizi ya msimu baada ya mapumziko ya wiki mbili,” akasema Harrisson.

Gor ilimaliza katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 46, alama 19 nyuma ya mabingwa wapya Tusker.

Ulimwengu, raia wa Burundi aliibuka mfungaji bora wa K’Ogalo kwa mabao manane na duru zinaarifu kuwa asharejea kwao Burundi kusaka timu nyingine.

Kwa upande mwingine, Okello, mzaliwa wa Uganda ambaye pia ana uraia wa Sudan Kusini, alifunga mabao matano kwenye ligi na idadi sawa na hiyo katika Kombe la Betway.

“Hata kabla ya mechi yetu ya mwisho ya Nzoia, sikufahamu walikokuwa wametoweka Okello na Jules. Hata hivyo, jambo muhimu ni kuwa sasa tunakisuka upya kikosi chetu kwa ajili ya msimu mpya na mechi za CAF. Lengo langu kama mkufunzi ni kushindia timu hii mataji mengi msimu ujao,” akaongeza Harrisson, raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 60.

Kando na Harrisson, Katibu Mkuu wa Gor Mahia Sam Ochola, pia alithibitisha kuwa wachezaji wengi watatimuliwa timuni ili kuwaleta wengine wakali zaidi.

“Tunataka timu yetu iipige hatua kwenye CAF na pia kushinda ubingwa tena. Mageuzi yaja timuni kulingana na mapendekezo ya kocha wetu mpya na nawaomba mashabiki wetu watuunge mkono katika hili,” akasema Ochola.

K’Ogalo ambayo inakumbwa na uchechefu wa hela tayari imenasa huduma za mnyakaji raia wa Mali Adama Keita, 31 ambaye usajili wake ulikashifiwa mno na mashabiki kutokana na ubora wa makipa Gad Mathews na Samuel Njau.

You can share this post!

Furaha mwanamume aliyetoweka miezi 8 iliyopita akirejea

Ruto avuliwa GSU