Michezo

Gor Mahia Youth, Butterfly na Tandaza zawika

June 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

GOR Mahia youth, Butterfly FC na Tandaza FC ziliendelea kufukuzana kwenye mechi za mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili baada ya kila moja kuvuna alama tatu muhimu.

Gor Mahia Youth ilidhalilisha Karatina Homeboys kwa magoli 9-2 kwenye patashika iliyopigiwa uwanjani City Stadium, Nairobi. Nao wanasoka wa Butterfly FC walibugiza Gathanga FC mabao 2-0 huku Tandaza FC ikitwaa ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya CMS Allstars Uwanjani Lower Kabete.

Wafungaji wa Butterfly FC walikuwa Jeremy Nyongesa na Musa Wamalwa walioitingia bao moja kila mmoja. Naye Levin Atulo alitikisa wavu mara mbili na kubeba Tandaza FC kujizolea alama zote muhimu.

Nayo Gor Mahia Youth ilizoa ufanisi huo kupitia Samuel Oluoch mabao manne, Lyodd Kavuchi alipiga mbili safi huku Arnold Kariuki na Keith Imbali wakitikisa wavu mara moja kila mmoja. Hata hivyo mchezaji wa Karatina Homeboys aliifaidi Gor Mahia Youth baada ya kujifunga kimakosa.

”Ushindi wetu unazidi kutuongezea tumaini la kufanya kweli,” ofisa wa Gor Mahia Youth, George Onyango alisema. Kwa kuvuna pointi 53 Gor Mahia Youth ingali kifua mbele. Tandaza ya pili kwa alama 44, sawa na Butterfly FC tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Nayo Gogo Boys iliilaza Mathaithi FC bao 1-0, Bomas of Kenya ilizimwa kwa mabao 2-1 na MKU Thika huku Spitfire ikizoa mabao 2-0 dhidi ya Wajiji FC.

Matokeo hayo yanafanya MKU Thika, Karatina Homeboys na Mathaithi United kusalia katika mduara wa nafasi tatu za kuteremshwa ngazi msimu ujao.