Michezo

Gor Mahia Youth na Butterfly zashindwa kupepea

June 3rd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Tandaza FC ilifanikiwa kurukia nafasi mbili bora wakati Butterfly FC na Gor Mahia Youth kila moja ikitema alama mbili muhimu baada ya kutoka sare tasa kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili iliyopigiwa Uwanja wa Shule ya Msingi ya Githunguri.

Nayo Bomas of Kenya ilijiongezea tumaini la kukwepa shoka la kushushwa ngazi baada ya Boniface Otieno kupiga moja safi na kuibeba kuzoa bao 1-0 mbele ya Karatina Homeboys. Tandaza FC ilipiga hatua ilipocharaza Gatanga FC mabao 3-1 kupitia Kevin Atulo, Byron Otieno na Walter Orando.

”Nashukuru vijana walionyesha ujasiri na kuhimili upinzani mkali lakini tulikubali yaishe,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema na kudokeza kuwa bado wanayo kazi nzito.

Kocha wa Butterfly FC, Bernard Shikuri (wa pili kulia) akizungumza na wachezaji wake kabla ya patashika yao na Gogo Boys kwenye mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili kusongeshwa mbele baada ya mvua kushuka dakika chache kabla ya kuingia mzigoni. Mchezo huo ulikuwa katika Uwanja wa Woodley Kibera, Nairobi. Picha/ John Kimwere

Naye ofisa wa Gor Mahia Youth, George Onyango alisema ”Dah! Kuachia alama mbili ni pigo kwetu lazima tujikaze kwenye mechi sijazo.”

Baada ya matokeo hayo, Gor Mahia Youth ingali inaendelea kuongoza kipute hicho kwa alama 46, sita mbele ya Tandaza. CMS Allstars ni ya tatu kwa alama 39, sawa na Butterfly tofauti ikiwa idadi ya mabao. Kwenye mechi nyingine, Kibra United ilitoshana nguvu mabao 2-2 na Spitfire.