Michezo

Gor Mahia Youth na Tandaza FC moto wa daraja ya pili

April 22nd, 2019 1 min read

NA JOHN KIMWERE

GOR Mahia Youth imezima Bomas of Kenya kwa mabao 5-0 wakati Karatina Homeboys ikidhalilishwa kwa magoli 7-1 na Tandaza FC kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili iliyochezewa Uwanjani Lower Kabete, Nairobi.

Matokeo hayo yalifanya Gor Mahia Youth kuendelea kukaa kifua mbele kwenye jedwali ya kipute hicho.

Hata hivyo wanasoka wa Tandaza wanatifua kivumbi kikali wakilenga kuwapiku limbukeni hao. Tandaza FC ya kocha, Kennedy Aluvisia ilifunza wenzao jinsi ya kucheza kandanda na kujizolea pointi tatu muhimu.

Tandaza FC ilifanikiwa kutesa wapinzani hao na kufanya kweli kupitia Geoffrey Adero na Kennedy Mutesa waliocheka na nyavu mara mbili kila mmoja huku Walter Orando, Byron Ochieng na Reuben Onsando kila mmoja akiitingia bao moja.

”Nashukuru vijana wangu kwa kuonyesha kazi nzuri na kuzima ndoto ya wenzetu,” kocha wa Tandaza alisema na kuwataka kutoleza kamba mbali wazidi kufanya kweli ili kujiongezea matumaini ya kuwapiku wapinzani wao na kuzoa tiketi ya kusonga mbele msimu ujao.

Naye Collins Mwanzi alipiga kombora moja safi na kubeba CMS Allstars kuzaba Kibra United kwa bao 1-0 kwenye mchezo uliochezewa Woodley Kibra, Nairobi.

Mathaithi FC iliachia alama zote baada ya kuingia mitini na kukosa kufika kiwanjani kucheza na Spitfire FC huku Gathanga ilitoshana nguvu bao 1-1 na Wajiji FC.