Michezo

Gor Mahia Youth wapiga Equity Bank na kutwaa taji

July 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Gor Mahia Youth imetwaa kombe la Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu wa 2018/2019 baada ya kufanya kweli kwenye mechi tatu za kutafuta bingwa wa kipute hicho.

Kikosi cha Gor Mahia Youth ambacho hunolewa na kocha, Tom Ogweno kilipapura Equity Bank FC 3-0 kabla ya kutoka sare tasa na Balaji EPZ.

Gor Mahia Youth iliibuka kidedea kwa kuzoa alama nne sawa na Balaji EPZ tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kuvuna mabao 2-1 kwenye mechi ya pili dhidi ya Equity Bank FC.

Gor Mahia Youth na Balaji EPZ zimepandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu ujao. Gor Mahia Youth ilipata ufanisi huo kupitia Alphonse Keith aliyetikisa wavu mara mbili na kuzoa goli la tatu baada ya mchezaji wa Equity Bank FC kujifunga.

Nao wafungaji wa Balaji EPZ walikuwa Caleb Omondi na Evans Juma waliocheka na wavu mara moja kila mmoja.

”Bila shaka napongeza wachezaji wangu kwa kazi njema ya msimu huu ambapo hatimaye tumefaulu kunasa tiketi ya kupandishwa daraja msimu ujao,” kocha huyo wa Gor Mahia Youth alisema.

Gor Mahia Youth ilishiriki mechi hizo baada ya kumaliza kileleni kwenye jedwali la mechi za Kundi C kwa alama 57, tisa mbele ya Butterfly FC. Kwa alama 46, Balaji EPZ ilimaliza kifua mbele Kundi A huku Equity Bank FC ikitwaa ubingwa wa Kundi B kwa kufikisha alama 50,11 mbele ya Kariobangi Sharks B.