Michezo

Gor Mahia Youth yapiga hatua

May 13th, 2019 1 min read

 Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Gor Mahia Youth iliendelea kuimarisha kampeni zake kufukuzia tiketi ya kusonga mbele, nayo Butterfly FC ilijikuta njia panda ilipozabwa mabao 2-1 na Bomas of Kenya kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili iliyopigiwa uwanja wa Bomas of Kenya.

Gor Mahia Youth ilisalia kileleni mwa ngarambe hiyo ilipobamiza Tandaza FC mabao 3-0 kupitia Samuel Oluoch, Lyodd Kavuchi na Keith Imbali walioitingia bao moja kila mmoja.

Gor Mahia Youth iliandikisha ushindi huo na kulipiza kisasi baada ya kubamizwa mabao 2-0 na Maafande wa Spitfire wiki moja iliyopita,.

”Hakika hatuelewi kinachoendelea tumepoteza alama tatu muhimu na kujikuta katika wakati mgumu kwenye jitihada zeti kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi msimu uja,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alifunguka na kuongeza kwamba hata hivyo kamwe hawatalegeza uzi.

Magoli ya Bomas of Kenya yalipatikana kupitia David Aura na Dan Oduor huku Ibrahim Chimwani akitingia Buttefly bao la kufuta machozi.

Katika msimamo wa kinyang’anyiro hicho, Gor Mahia Youth inaendelea kuongoza kwa kufikisha pointi 44, Tandaza imeshikilia mbili kwa kuzoa alama 36, moja mbele ya Butterfly FC.

Kwenye mfululizo wa michuano hiyo, wanasoka wa Wajiji FC walinyukwa mabao 4-2 na Karatina Homeboys, Kibra United ililizwa bao 1-0 na MKU Thika, CMS Allstars ilikanyanga Mathaithi FC mabao 3-2 huku Gogo Boys ikishindwa kutamba katika ardhi ya nyumbani na kutoka sare dhidi ya Gathanga FC uwanjani Woodley Kibra, Nairobi.