Michezo

Gor, Nzoia, Chemelil na Sofapaka zawika KPL

March 4th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KWA wiki ya pili mfululizo, timu zimeendelea kutawala mechi zao za nyumbani baada ya wenyeji Gor Mahia, Nzoia Sugar, Chemelil Sugar na Sofapaka kuwika Jumamosi.

Mabingwa mara 16 Gor, ambao wananolewa na Muingereza Dylan Kerr, wamenyuka Bandari 2-0 kupitia mabao ya beki wa Bandari Felly Mulumba (alijifunga) na mshambuliaji Meddie Kagere uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Mechi iliyotanguliwa kusakatwa uwanjani humu katika ya Sofapaka na wageni Posta Rangers ilishuhudia wenyeji wakitamba 2-1 kupitia mabao ya Stephen Waruru na Kepha Aswani. Rangers ilipata bao la kujiliwaza kutoka kwa Gearson Likono.

Mjini Chemelil, wageni Zoo Kericho walizamishwa 2-1 kupitia mabao ya Emmanuel Jacobs (penalti) na John Kuol. Kepha Ondati alifungia Zoo.

Nzoia Sugar ilivuna ushindi mkubwa Jumamosi kwa kulemea Kakamega Homeboyz 3-1 uwanjani Sudi mjini Bungoma. Elvis Rupia alifungia Nzoia mabao yote naye Kikoyo Hassan akapachika bao la Homeboyz.

Vihiga United pekee haikushinda nyumbani baada ya kukabwa 0-0 na Nakumatt uwanjani Bukhungu mjini Kakamega.

Matokeo (Machi 3):

Chemelil Sugar 2-1 Zoo Kericho

Sofapaka 2-1 Posta Rangers

Nzoia Sugar 3-1 Kakamega Homeboyz

Vihiga United 0-0 Nakumatt

Gor Mahia 2-0 Bandari

Ratiba (Machi 4):

SoNy Sugar vs. AFC Leopards (3.00pm)

Thika United vs. Mathare United (3.00pm)

Ulinzi Stars vs. Tusker (3.00pm)

Wazito vs. Kariobangi Sharks (3.00pm)