Gor roho mkononi ikibainika kocha Harrison hatarejea

Gor roho mkononi ikibainika kocha Harrison hatarejea

Na CECIL ODONGO

MASHABIKI wa Gor Mahia wameingiwa na wasiwasi kuwa Kocha wa Mark Harrison ambaye alienda likizoni kwao Uingereza huenda akakosa kurejea kuendelea kunoa timu hiyo mnamo Januari.

Harrison aliabiri ndege baada ya kichapo cha 2-1 mikononi mwa Kakamega Homeboyz Jumamosi iliyopita siku chache baada ya mkewe ambaye amekuwa akiishi naye hapa Kenya pia kurejea Uingereza.Ingawa ni msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya, mashabiki wa K’Ogalo wameingiwa na wasiwasi kuwa Harrison huenda hatarejea kufunza Gor ambayo inakabiliwa na uchechefu wa kifedha.

Wakufunzi wa kigeni wamekuwa wakija Gor kisha kuondoka kwenda likizo kwao kisha wao hujiuzulu wakiwa makwao, jambo ambalo limeibua wasiwasi kuwa Harrison huenda akafuata mkondo huo.Aliyekuwa Kocha Steve Polack, Dylan Kerr, Hassan Oktay na Ze Maria wote waliondoka na kuenda likizo ila hawakurudi, wakiamua kujiuzulu wakiwa ugenini.

Gor ambayo mechi yao dhidi ya Posta Rangers iliyofaa kusakatwa jana iliahirishwa, ina kibarua kigumu dhidi ya Nairobi City Stars mnamo Disemba 30 bila Harrison huku Naibu Kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo akitarajiwa kuwaongoza kwenye mechi hiyo.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Ray Oruo alieleza Taifa Leo kuwa hawana deni lolote la Harrison ila kocha huyo amekuwa akilalamikia presha kutoka kwa mashabiki na uongozi wa klabu hiyo ili kupata matokeo bora.“Ndiyo kocha ameelekea likizo na tulimpa ruhusa hiyo.

Tuna matumaini kuwa atarejea japo katika siku zimepita amekuwa akiteta kuwa hataki presha kutoka kwa mashabiki na uongozi wa klabu. Wajua hiyo ni ngumu hasa wakati huu mashabiki wamerejea uwanjani na unajua jinsi wao husukuma timu ipate matokeo mazuri,” akasema Oruo.

Kando na kichapo mikononi mwa Homeboyz, Gor ilikuwa imeenda sare tasa dhidi ya Bandari majuma mawili yaliyopita. Kando na hayo, timu hiyo ilibanduliwa kwenye Kombe la Mashirikisho Afrika 9CAF) na AS Otoho d’Oyo.

You can share this post!

Maluda Super Cup yatinga nusu-fainali

Asike imani tele Tusker itaibwaga Homeboyz

T L