Michezo

Gor, Tusker wajikita kileleni Homeboyz, Ulinzi wakipaa

January 7th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KAKAMEGA Homeboyz, Ulinzi Stars na Kariobangi Sharks zimepiga hatua moja mbele kila mmoja baada ya kuzoa alama muhimu katika mechi za kufungua mwaka wa 2020 wikendi.

Mabingwa watetezi Gor Mahia na washindi wa zamani Tusker wanasalia katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 32 na 31 mtawalia. Viongozi Gor walibwaga Wazito 1-0 nao wanamvinyo wa Tusker wakaandikisha ushindi mkubwa msimu huu wa mabao 7-0 dhidi ya Chemelil Sugar.

Homeboyz, ambayo itafufua uhasama dhidi ya Gor mnamo Januari 12, imepaa nafasi moja hadi nambari tatu baada ya kulipua Kisumu All Stars 4-0.

Uadui kati ya Gor na Homeboyz ulianzishwa na mmiliki wa Homeboyz, Cleophas ‘Toto’ Shimanyula alipojipiga kifua kabla ya mechi ya mkondo wa kwanza mwezi Novemba kuwa timu yake itakanyaga vijana wa Steven Polack kabla ya kulimwa 3-0.

Homeboyz imezoa alama 30, mbili zaidi na Ulinzi, ambayo pia ilikuwa na wikendi nzuri ilipokung’uta Posta Rangers na kurukia nafasi ya nne kutoka nambari tano. Gor imesakata mechi 13 nazo Tusker, Homeboyz na Ulinzi zimecheza mechi mbili zaidi.

Western Stima, ambayo haikucheza wikendi, imetupwa hadi nambari tano. Wanaumeme wa Stima wamezoa alama 27 kutokana na mechi 14.

Hakuna mabadiliko ya nafasi kutoka nambari sita hadi 13, ingawa KCB, AFC Leopards, Sofapaka, Mathare United na Bandari, zilijiongezea alama muhimu.

Wanabenki wa KCB wamekwamilia nafasi ya sita baada ya kutoka 1-1 dhidi ya Mathare na kufikisha alama zao kuwa 26.

Leopards inafuata kwa alama 25 baada ya kupepeta Zoo 4-1. Sofapaka ilikabwa 2-2 dhidi ya Kariobangi Sharks na kusalia katika nafasi ya nane kwa alama 22, moja mbele ya nambari tisa Mathare.

KCB, Sofapaka na Mathare zimecheza mechi 14 nayo Leopards imeingia uwanjani mara 15. Rangers, ambayo haina ushindi katika mechi tano mfululizo, inafunga mduara wa 10-bora kwa alama 19 kutokana na mechi 15.

Baada ya kupata ushindi wa bwerere kutokana na Nzoia Sugar kukosa kufika uwanjani wikendi, Bandari sasa ina jumla ya alama 18. Inashikilia nafasi ya 11.