Michezo

Gor wachupa kileleni KPL

December 13th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Gor Mahia walidumisha rekodi yao ya kutoshindwa na Zoo Kericho hadi mechi tano kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Kenya (KPL) baada ya kuwachabanga 4-0 na kurukia juu ya jedwali Jumatano.

Mabao ya raia wa Ivory Coast Ephrem Guikan katika dakika ya kwanza na 16 pamoja na moja kutoka kwa Samuel Onyango dakika ya 39 na Mganda Erisa Ssekisambu dakika ya 72 yalitosha kuzamisha chombo cha Zoo, ambayo ililimwa na Gor 4-2 nyumbani na 4-1 ugenini msimu uliopita.

Mabingwa mara 17 Gor, ambao wananolewa na kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno, wanaongoza ligi hii ya klabu 18 kwa alama tatu. Wameng’oa mabingwa wa mwaka 2008 Mathare United kileleni kwa tofauti ya magoli. Gor itaalika Lobi Stars ya Nigeria jijini Nairobi katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika hapo Desemba 16. Zoo inavuta mkia ligini.

Gor na Zoo zimesakata mechi moja zaidi ya timu hizo zingine 16. Ligi itaendelea Desemba 15-16. Mabingwa wa Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya almaarufu SportPesa Shield, Kariobangi Sharks pia hawatakuwa na mechi ya ligi wikendi hii. Sharks itaalika miamba wa Ghana, Asante Kotoko jijini Nairobi mnamo Desemba 15 katika mechi ya Kombe la Mashirikisho (Confederation Cup). Kotoko iliwasili jijini Nairobi hapo Desemba 12.

Msimamo wa Ligi Kuu ya Kenya

                           MP     W    D     L    GF    GA   P

Gor Mahia       2      1      0      1      5      2      3

Mathare Utd.   1      1      0      0      2      0      3

Vihiga Utd.       1      1      0      0      2      0      3

Sofapaka 1      1      0      0      2      1      3

Bandari    1      1      0      0      2      1      3

Western Stima 1      1      0      0      1      0      3

Kakamega Homeboyz     1      1      0      0      1      0      3

Nzoia Sugar     1      1      0      0      1      0      3

Tusker     1      0      1      0      1      1      1

Leopards 1      0      1      0      1      1      1

SoNy Sugar     1      0      1      0      1      1      1

Kariobangi Sharks   1      0      1      0      1      1      1

Mount Kenya Utd.   1      0      0      1      1      2      0

KCB 1      0      0      1      0      1      0

Posta Rangers 1      0      0      1      0      1      0

Ulinzi Stars      1      0      0      1      0      2      0

Chemelil Sugar        1      0      0      1      0      2      0

Zoo  2      0      0      2      0      5      0