Michezo

Gor waendea Zoo, Tusker ikiwaalika Sharks gozini KPL

March 27th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA watetezi na wafalme mara 17 wa Ligi Kuu ya KPL, Gor Mahia watakuwa leo Jumatano wageni wa Zoo mjini Kericho katika mchuano unaotarajiwa kuzidisha ushindani kileleni mwa jedwali la kipute hicho.

Gor Mahia watadhibiti usukani wa kivumbi hicho iwapo wataibuka na ushindi nao Sofapaka na Bandari wajikwae dhidi ya Mount Kenya United na Kakamega Hoemboyz mtawalia.

Bandari watakuwa wenyeji wa Homeboyz katika uwanja wa Mbaraki Sports Club jijini Mombasa huku Sofapaka waliotawazwa mabingwa wa KPL mnamo 2009 wakiwaalika Mt Kenya United ugani Kenyatta, Machakos.

Hadi kufikia sasa, Sofapaka wanaselelea kileleni mwa jedwali la KPL kwa alama 33 sawa na Bandari ambao wanashikilia nafasi ya pili kutokana na uchache wa mabao.

Gor Mahia ambao wana michuano mitatu zaidi ya kusakata ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na wapinzani wao wakuu, wanafunga orodha ya tatu-bora kwa alama 32.

Ni pengo la alama moja pekee ndilo linalodumu kati ya Gor Mahia na Mathare United walionyanyua ubingwa wa KPL kwa mara ya mwisho mnamo 2008 chini ya mkufunzi wao wa sasa, Francis Kimanzi.

Katika mchuano mwingine unaotarajiwa kuwa wa kusisimua zaidi, Tusker ambao ni mabingwa mara 11 watakuwa wenyeji wa Kariobangi Sharks katika uwanja wa Ruaraka.

Alama tatu kwa Tusker zitawavusha hadi nafasi ya saba kwa alama 26 iwapo Western Stima watashindwa kutamba dhidi ya wanabenki wa KCB katika mchuano wa pili utakaoandaliwa uwanjani Kenyatta, Machakos.

Chini ya kocha Robert Matano, Tusker kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa huku Sharks ya mkufunzi William Muluya wakifunga mduara wa tano-bora kwa pointi 29.

Ulinzi Stars ambao kwa sasa wanaanza maisha chini ya kocha wa zamani Benjamin Nyangweso, watakuwa wenyeji wa mabingwa wa 2006 SoNy Sugar ugani Afraha, Nakuru.

Iwapo watatumia vyema uwanja wao wa nyumbani na kuibuka na ushindi, basi Ulinzi wataruka hadi nambari ya nane kwa alama 25 jedwalini.

Kufikia sasa, wanajeshi hao wamejizolea pointi 22 pekee baada ya kusajili ushindi mara nne, kuambulia sare 10 na kupoteza mechi tatu kutokana na jumla ya michuano 17 iliyopita. SoNy Sugar wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 28.

Kwingineko, Vihiga United watawaalika AFC Leopards kwa gozi kali uwanjani Bukhungu, Kakamega. Mchuano huo utakuwa jukwaa mwafaka zaidi kwa Leopards ya kocha Casa Mbungo kujinyanyua zaidi na kujikweza pazuri jedwalini.

Ratiba ya KPL (Leo Jumatano):

Sofapaka na Mt Kenya United (Machakos)
Vihiga Utd na AFC Leopards (Kakamega)
Zoo na Gor Mahia (Kericho)
Bandari na KK Homeboyz (Mombasa)
Tukser na Sharks (Ruaraka)
Ulinzi Stars na SoNy Sugar (Nakuru)
KCB na Western Stima (Machakos)