Michezo

Gor wainyeshea Assad 5-1 kwenye SportPesa Shield

May 28th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara 10 wa Kombe la Rais, Gor Mahia walitinga raundi ya 32-bora ya kombe hili almaarufu sasa kama SportPesa Shield, kwa kunyamazisha SS Assad kwa mabao 5-1 mjini Mombasa, Mei 27, 2018.

Gor, ambayo mara ya mwisho ilishinda shindano hili la muondoano ni mwaka 2012, ilibandua nje Assad kupitia mabao ya Lawrence Juma (mawili), Godfrey Walusimbi, Eliud Lukowam na Jacques Tuyisenge. Tumaini Mussa alifungia Assad bao la kufutia machozi.

Gor itakutana na mshindi kati ya KenPoly na Savannah Cement katika raundi ya 32-bora. Mechi 31 za raundi ya 64-bora zitasakatwa kati ya Juni 1 na Juni 3.

Vijana wa kocha Dylan Kerr, Gor, watarejelea mechi za Ligi Kuu kesho watakapomenyana na SoNy Sugar mjini Awendo. Mabingwa wa Ligi Kuu mara 16, Gor, wataanza mchuano huu na asilimia kubwa ya kuibuka washindi. M

ara ya mwisho walipoteza dhidi ya SoNy ilikuwa 1-0 Agosti 25 mwaka 2011. SoNy pia wamekuwa wakisikitisha ligini msimu huu.