Michezo

Gor wasonga mbele CAF Champions League baada ya kupiga APR 3-1 jijini Nairobi na kuwadengua kwa jumla ya mabao 4-3

December 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MABAO mawili ya dakika za mwisho kutoka kwa Sydney Ochieng na Nicholas Kipkirui yalisaidia Gor Mahia kupokeza APR ya Rwanda kichapo cha 3-1 katika Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) mnamo Disemba 5, 2020.

Ushindi huo uliosajiliwa na Gor Mahia katika uwanja wa Nyayo, Nairobi uliwabandua APR kwenye kipute hicho kwa jumla ya mabao 4-3. APR walijibwaga uwanjani wakijivunia ushindi wa 2-1 kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezewa jijini Kigali mnamo Novemba 28, 2020.

Chini ya kocha mshikilizi Sammy ‘Pamzo’ Omollo, Gor Mahia kwa sasa wanafuzu kwa raundi ya kwanza ya kuwania taji la CAF ambapo watakutana ama na El Nasr ya Libya au mabingwa wa Algeria, CR Belouizdad.

Wakicheza dhidi ya Gor Mahia katika mkondo wa pili, APR walipata penalti katika dakika ya nane baada ya Andrew Juma kumchezea visivyo Jacques Tuyisenge ambaye alimpoteza mkwaju huo uliopanguliwa na kipa Gad Matthews. Samuel Onyango aliwafungulia Gor Mahia ukurasa wa mabao katika dakika ya 18.

Bao la Onyango liliwapa Gor Mahia motisha zaidi ya kuvamia lango la wageni wao japo kipa Ndayisenga Rwabugiri alijitahidi kudhibiti vilivyo makombora aliyoelekezewa na Benson Omal na Bernard Ondiek.

Presha hiyo kutoka kwa Gor Mahia iliwaweka APR katika ulazima wa kufanya mabadiliko ya mapema yaliyoshuhudia Yannick Bizimana akijaza nafasi ya Claude Niyamugabo katika dakika ya 31.

Gor Mahia walianza kipindi cha pili kwa matao ya juu na huku kocha Pamzo aliwaleta uwanjani Cliffton Miheso na Sydney kujaza nafasi za Tito Okello na Ondiek.

Kasi iliyochangiwa na wawili hao kwenye safu ya mbele ya Gor Mahia iliwalazimu APR pia kufanya mabadiliko ya haraka yaliyoshuhudia Deudone Ndayishimiye na Keddy Nsanzimfura wakiondolewa na nafasi zao kutwaliwa na Claude Byiringiro na Djabel Manshimiye.

Kuja kwa Geoffrey Ochieng aliyejaza nafasi ya Onyango katika nafasi ya 82 ulilegeza safu ya kati ya Gor Mahia na hivyo kuwapa APR upenyo wa kusawazisha mambo kupitia kwa Nsanzimfura katika dakika ya 83.

Bao hilo lilimchochea Pamzo kufanya mabadiliko ya haraka yaliyoshuhudia Kipkirui akiingia uwanjani kuchukua nafasi ya nahodha Kenneth Muguna aliyekuwa akichechemea baada ya kupata jeraha.