Michezo

Gor yaibwaga Ingwe kuchuana na Hull City Mei 13

May 1st, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

GOR Mahia imeimarisha rekodi yake ya kutoshindwa na AFC Leopards hadi mechi tano baada ya kuichapa kwa njia ya penalti 5-4 Jumanne na kunyakua tiketi ya kumenyana na Hull City hapo Mei 13, 2018.

Mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor na mabingwa mara 13 Leopards walimaliza dakika 90 za mchuano huu wa kusisimua bila kufungana uwanjani Afraha mjini Nakuru.

Gozi hili la 85 katika ya klabu hizi kongwe nchini Kenya lilishuhudia Mrwanda Jacques Tuyisenge akipoteza penalti ya kwanza kwa upande wa Gor sawa na mwenzake kutoka Leopards, Whyvonne Isuza.

Gor haikupoteza tena penalti, huku Mrwanda Meddie Kagere, Mganda Godfrey Walusimbi na George ‘Blackberry’ Odhiambo, Joachim Oluoch na Ben Ondiek wakimwaga kipa wa Leopards, Ezekiel Owade. Kipa wa Gor, Shaban Odhoji alipangua penalti ya Isuza, lakini akashindwa kupangua penalti za mchezaji bora wa mwezi Machi, Ezekiel Odera pamoja na Duncan Otieno, Robinson Kamura na Mganda Baker Lukooya. Penalti ya mwisho ya Leopards ilipigwa nje na Vincent Oburu.

Hull, ambayo inashiriki Ligi ya Daraja ya Pili ya Uingereza, itasakata mechi yake ya mwisho ya ligi hiyo Mei 6 dhidi ya Brentford kabla ya kuzuru Kenya.

Itakabiliana na Gor katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi mnamo Mei 13.

Ni mara ya pili Gor inacheza dhidi ya timu kutoka Uingereza baada ya kulemewa 2-1 na Everton jijini Dar es Salaam, Tanzania, mwaka 2017.

Gor ilinyuka Leopards 3-0 na kunyakua tiketi ya kumenyana na Everton.

Hull pia si timu geni kwa Wakenya. Ilizaba timu ya mstaa kutoka Ligi Kuu ya Kenya (SportPesa All Stars) 2-1 uwanjani K-COM nchini Uingereza mnamo Februari 27, 2017.

Hull, Gor na Leopards zinapata udhamini kutoka kwa kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa. Mwaka 2016, SportPesa ilitangazwa wadhamini wakuu wa Hull baada ya kusaini kandarasi ya misimu mitatu (2016/17, 2017/18 na 2018/19).

Leopards na Gor zilisaini kandarasi ya miaka mitatu na SportPesa zaidi ya wiki moja iliyopita ya udhamini wa Sh156.4 milioni na Sh198.6 milioni, mtawalia.