Michezo

Gor yajinyanyua kwa kupiga Zoo 4-1

October 4th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

GOR Mahia imeandikisha ushindi wake wa kwanza katika mechi tano kwenye Ligi Kuu baada ya kupondaponda Zoo Kericho kwa mabao 4-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Alhamisi.

Vijana wa kocha Dylan Kerr, ambao walitawazwa rasmi mabingwa wa msimu 2018 walipotoka 2-2 dhidi ya Mathare United uwanjani Moi mjini Kisumu mnamo Septemba 30, walizamisha Zoo kupitia mabao ya Wesley Onguso, Wellington Ochieng’, Bernard Ondiek na raia wa Burundi Francis Mustapha. Mwanasoka bora wa Kenya mwaka 2017 Michael Madoya alifungia Zoo bao la kufuta machozi.

Gor, ambayo inajivunia mataji 17 ya ligi, ina alama 75 kutokana na mechi 33. Itakamilisha msimu dhidi ya mabingwa mara 11 Tusker mnamo Oktoba 7. Zoo itafunga msimu wake wa pili mfululizo kwenye Ligi Kuu dhidi ya mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka mnamo Oktba 7. Kabla ya kupiga Zoo, Gor ilikuwa imepoteza mechi nne na kupiga sare moja katika mashindano yote.

Ligini, ilichapwa 1-0 na Thika United mnamo Septemba 16, ikapepetwa 2-0 na mabingwa mara nne Ulinzi Stars mnamo Septemba 19 na kunyamazishwa 2-0 na washiriki wapya Vihiga United mnamo Septemba 26 kabla ya kukabwa 2-2 na washindi wa mwaka 2008 Mathare United. Zoo inashikilia nafasi ya 11 kwa alama 41 kwenye ligi hii ya klabu 18, ambayo itatamatika Oktoba 7.