Michezo

Gor yakanusha kumuuza mshambulizi wa Ivory Coast

November 14th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MABINGWA mara 17 wa ligi ya KPL nchini Gor Mahia wametangaza kwamba mshambulizi Ephraim Guikan raia wa Ivory Coast bado ni mchezaji wao wala hawajamuuza au kumwondoa kwenye mipango yao jinsi inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari na taarifa za mitandao.

Mshambulizi huyo pande la raia, aliwafungia K’Ogalo mabao 13 msimu uliokamilika wa 2017/18 na uvumi umekuwa ukienea kwamba aliwasilisha barua kwa usimamizi wa Gor Mahia akitaka kuruhusiwa kutafuta klabu nyingine.

Vile vile Guikan kupitia mtandaoni alimkashifu vikali afisa moja wa ngazi ya juu klabuni humo kwa kuharibu taaluma yake ya soka akiwa na Sirkal hali inayofasiriwa na jinsi alivyosugua benchi KPL ikilekea kukamilika,  kukosa kumnyang’anya namba Jacques Tuyisenge na kukosa kung’aa kwenye mechi za K’Ogalo za CAF.

Hata hivyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa mabingwa hao watetezi wa KPL Omondi Aduda amejitokeza na kuthibitisha kwamba Guikan bado ana kandarasi na klabu hiyo inayomruhusu kuwasakatia hadi mwaka wa 2019.

Huku msimu wa KPL 2018/19 ukitarajiwa kuanza mwezi Disemba, Gor Mahia tayari wametwaa huduma za mwanasoka  wao wa zamani Kenneth Muguna, Shafik Batambuze kutoka Singida United na Nicholas Kipkirui aliyekuwa akiwajibikia Zoo Kericho kama mbinu ya kuimarisha kikosi chao wanapojisuka upya  ili kutamba msimu huo.

Majagina hao pia wamerefusha mkataba wa mnayakaji wa nambari moja Boniface Oluoch wanapojitayarisha kuvaana na Nyasa Big Bullets ya Malawi kwenye mechi ya kuwania klabu bingwa barani Afrika(CAF) Novemba 28 2018.

Mkondo wa kwanza wa mechi hiyo utasakatwa katika uga wa MISC Kasarani kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye ugani Kamuzu, Wilaya ya Blantyre nchini Malawi.