Gor yarejea kileleni, Vihiga Bullets ikisimamisha AFC

Gor yarejea kileleni, Vihiga Bullets ikisimamisha AFC

Na CECIL ODONGO

GOR Mahia jana Jumapili ilirejea hadi kileleni mwa msimamo wa jedwali la Ligi Kuu licha ya kupata sare tasa dhidi ya Bandari katika mechi iliyosakatwa katika uga wa kitaifa wa Nyayo.

Mabingwa watetezi Tusker ambao walikuwa wakirejea ligini kwa mara ya kwanza baada ya kubanduliwa kwenye Kombe la Mashirikisho (CAF) wikendi iliyopita, pia waliagana sare ya kutofungana dhidi ya Sofapaka katika uga wa Ruaraka.

Wavuta mkia Vihiga Bullets nao walipata sare yao ya pili msimu huu, ikiwa 1-1 dhidi ya AFC Leopards ugani Bukhungu. Eugene Mukangula alipoiweka AFC Leopards uongozi kunako dakika ya 75 kabla ya Mike Isabwa kusawazishia Bullets kupitia penalti dakika ya 89.

Mvamizi wa Bullets Godfrey Airo alipiga shuti kali ambayo Mukangula alinawa katika eneo la hatari na kusababisha mkwaju huo wa penalti.

Katika mechi ya pekee iliyoshuhudia ushindi, wenyeji KCB walilemea Ulinzi Stars 2-0 katika uga wa MISC Kasarani na kuzidisha shinikizo kwa wanajeshi hao ambao sasa hawajaonja ushindi katika mechi nne zilizopita.

Licha ya sare dhidi ya Bandari, Gor ilipaa hadi kileleni mwa msimamo wa jedwali kwa alama 18 sawa na Kakamega Homeboyz ambayo inadunishwa na uchache wa mabao, timu zote zikiwa zimecheza mara nane.

Tusker ambayo imeshinda mechi mbili pekee nayo inazidi kupata wakati mgumu kutetea ubingwa wao ikiwa katika nafasi ya 14 kwa alama saba baada ya mechi sita.

Mabingwa wa 2009, Sofapaka nao walipaa hadi nafasi ya nane kwa alama 14 baada ya kujibwaga uwanjani mara tisa.

Ugani MISC Kasarani, Michael Oduor aliwapa KCB uongozi dakika ya 19 kabla ya Derick Otanga kuongeza la pili dakika ya 82 na kufunga bao lake la nne msimu huu kuzamisha kabisa chombo cha Ulinzi Stars.

KCB sasa imepaa hadi nafasi ya pili kwa jedwalini kwa alama 18 baada ya mechi tisa huku ikiwa ya 10 kwa alama 12 baada ya mitanange minane.

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Okwalo ni mtunzi na mwalimu stadi

Tundo mfalme mpya mbio za magari nchini

T L