Michezo

Gor yasema haina deni lolote na mvamizi stadi Oliech

February 28th, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

USIMAMIZI wa miamba wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia umekanusha vikali madai yaliyoenezwa na vyombo vya habari kuwa mshambulizi Dennis Oliech alikuwa amegoma kucheza kwa kutolipwa mshahara na sehemu ya fedha za usajili wake.

Katika mahojiano ya kina na Taifa Leo Dijitali, Afisa Mkuu Mtendaji wa K’Ogalo Ludovic Aduda alisema habari zilizochapishwa magazetini na kuenezwa mtandaoni ni uongo mtupu na kudai hakujawahi kuwa na utata wowote kuhusu malipo ya Oliech.

“Tumesikitishwa sana na habari hizi ambazo ni uongo na walioziandika hawakuona haja ya kupata kauli yetu kabla ya kuzichapisha au kuzieneza. Oliech hakuwa kwenye kikosi cha wachezaji 20 wa kucheza mechi ya CAF mnamo Jumapili kwasababu kocha Hassan Oktay alimwaacha nje. Baada ya mechi hiyo amekuwa akifanya mazoezi na timu na hatuelewi kiini cha porojo zinazoenezwa. Mchezaji kutojumuishwa kikosini ni kawaida,” akasema Aduda.

Aidha, alifunguka na kusisitiza kwamba wanaheshimu mkataba kati yao na nyota huyo wa zamani wa Harambee Stars huku akidai kuwa hawana deni la mshambuliaji huyo tangu atue kambini mwao.

“Oliech amelipwa mshahara wa Januari na sehemu za fedha za usajili wake jinsi ilivyonakiliwa kwenye mkataba aliosaini. Hata Sh100,000 kwa kila mchezaji alizoahidi mwenyekiti Ambrose Rachier kwa kufuzu hatua ya makundi amelipwa ilhali jina lake halikuwa limewasilishwa kwa CAF,” akaongeza afisa huyo.

Ingawa hivyo, Aduda alisema kama klabu wanaheshimu na kuthamini kila mchezaji timuni japo inasikitika kuwa kuna baadhi ya watu wanaokerwa na uthabiti wa klabu hiyo wenye nia ya kuibua taharuki bila sababu zenye mashiko.

“Gor kwa sasa ni thabiti lakini kuna wadau wa soka ambao hawalali wakilenga kubuni mambo ambayo hayapo ili kuharibia klabu sifa. Lengo lao hata hivyo halitafaulu wala wachezaji wetu hawatapoteza dira. Tutaendelea kuwajibika tukilenga kushinda kila mechi,” akasisitiza Aduda.