Michezo

Gor, Zoo kuchezea Afraha nao Bandari wakialika Posta

October 3rd, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO na ABDULRAHMAN SHERIFF

MCHUANO wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) uliokuwa uwakutanishe Gor Mahia na Zoo Kericho mwishoni mwa wiki hii uwanjani Kenyatta, Machakos sasa utatandazwa katika uga wa Afraha, Nakuru.

Kwa mujibu wa waratibu wa kipute hicho, muda wa kupulizwa kwa kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi hiyo pia umebadilishwa kutoka saa kumi na robo jinsi ilivyokuwa imepangwa awali hadi saa tisa alasiri.

Kivumbi kingine ambacho kimeratibiwa upya na waendeshaji wa Ligi Kuu ya KPL ni kile kilichokuwa kiwakutanishe mabingwa wa 2009 Sofapaka na Bandari FC mnamo Jumapili.

Mchuano huo uliokuwa uanze saa nane kamili sasa utang’oa nanga saa tisa katika uwanja wa Kenyatta, Machakos.

Mechi ya Gor Mahia itakuwa ya pili kwa mabingwa hao watetezi wa KPL tangu wabanduliwe kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).

Chini ya kocha mpya Steve Polack, Gor Mahia walichuana jana na Nzoia Sugar uwanjani Mumias Sports Complex.

Kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Sofapaka, Bandari wanaopigiwa upatu wa kunyanyua ufalme wa KPL msimu huu watakuwa leo wenyeji wa Posta Rangers uwanjani Mbaraki Sports Club, Mombasa. Mchuano huu utakuwa wa kwanza kwa washikilizi hawa wa taji la Shield Cup kushiriki ligini tangu wawabandue Ben Guerdane kutoka Tunisia kwenye kampeni za Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF Confederations Cup).

Kufikia sasa, Bandari wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama saba sawa na Tusker FC, Ulinzi Stars, Kakamega Homeboyz na AFC Leopards ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la KPL.

Baada ya kuanza kampeni za msimu huu kwa sare tasa dhidi ya Mathare United waliotawazwa wafalme wa KPL mnamo 2008, Bandari waliwapepeta Zoo Kericho 3-2 katika mechi yao ya pili ligini.

Kwa upande wao, Rangers wanashikilia nafasi ya 13 jedwalini kwa alama nne sawa na Sofapaka waliopepetwa 2-1 na Rangers.

katika mchuano wa ufunguzi wa msimu huu. Tangu wakati huo, kikosi hicho cha mkufunzi Sammy Omollo kitakuwa kikipania leo kusajili ushindi wa kwanza ligini. Katika mechi yao ya pili, Rangers walilazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Homeboyz kabla ya chombo chao kuzamishwa kwa 1-0 na Western Stima.

Halaiki ya wapenda kandanda wa Mkoa wa Pwani wanatarajiwa kufurika leo uwanjani Mbaraki Sports Club kuishangilia timu yao ya Bandari FC ikicheza na Rangers ligini.

Mashabiki hao watafika kwa wingi ili kuwapongeza wanasoka wao kwa kufuzu kwa raundi nyingine Caf Confederation Cup baada ya kuitoa Ben Guerdane ya Tunisia wiki iliyopita. Pia watafika hapo uwanjani kuwapa motisha washinde pambano lao dhidi ya Rangers.

Kazi nzuri

Mkurugenzi wa Ufundi wa Admiral Youth FC, Aref Baghazally aliwaomba wapenda kandanda wajitokeze kwa wingi hapo Mbaraki leo Alhamisi kuishangilia timu yao iliyofanya kazi nzuri kwa kufuzu kwa raundi nyingine ya shindano la Caf.

“Tunastahili kuwapongeza wachezaji wetu kwqa kazi nzuri waliyoifanya na pia tutawawajibika kuipongeza timu yetu hii kwenye mechi zao za Ligi Kuu pamoja na mashindano ya barani Afrika ya Caf,” akasema Baghazally.

Bandari itacheza mchezo huo ukiwa ni watatu wa ligi kuu kwa siku mbili tu baada ya kuwasili kutoka Tunisia na inaopigania kushindas ipate kuhifadhi rekodi yake ya kutofungwa tangu ligi hiyo ianze. Hapo awali Bandari ilitoka sare ya 0-0 na Mathare United, ikazishinda Zoo Kericho 3-2 na SoNy Sugar 1-0.

Juhudi za kumpata Kocha Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala hazikufua dafu kwani simu yake ilikuwa imezima. Naibu wake Ibrahim Shikanda pia hakupatikana kuzungumzia juu ya mechi yao ya huko Tunisia na mchezo wao wa kesho dhidi ya Posta Rangers.

Mashabiki wa nyumbani wana tamaa kubwa ya timu yao ya Bandari kuopata ushindi. Baada ya mechi hiyo, Bandari itasafiri hadi jijini Nairobi kwa mchezo wao na Sofapaka FC hapo Jumapili.