Michezo

Goretzka ainusuru Ujerumani kupigwa

March 22nd, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

BERLIN, Ujerumani

LEON Goretzka alisaidia kocha Joachim Loew kukwepa kichapo alipofungia Ujerumani bao la kusawazisha 1-1 katika kipindi cha pili katika mechi ya kirafiki dhidi ya Serbia, Jumatano.

Baada ya kuwatema wachezaji wazoefu Jerome Boateng, Mats Hummels na Thomas Mueller kutoka timu ya taifa wiki mbili zilizopita, Loew alitangaza kuwa ilikuwa mwanzo wa enzi mpya kabla ya mchuano wa Jumatano.

“Kwa jumla, nilifurahia matokeo. Ni wazi kulikuwa na matatizo kadhaa katika mawasiliano, lakini hali hii huimarika wachezaji wanapoendelea kupata ujuzi katika kiwango hiki,” Loew aliambia runinga ya RTL nchini Ujerumani baada ya mechi.

Kikosi cha Ujerumani kilicho na wachezaji walio na umri mdogo kilionekana tulivu katika dakika za mwanzo, lakini Serbia ilipata bao kutokana na nafasi ya kwanza waliyopata dakika ya 12.

Mpira ulioguswa baada ya kona kupigwa ulimpata Luka Jovic peke yake mbele ya goli, na mvamizi huyo wa Eintracht Frankfurt akamwaga kipa Manuel Neuer.

Ujerumani ilipumzisha Kai Harvetz na Julian Brandt na kujaza nafasi zao na Marco Reus na Goretzka katika kipindi cha pili. Mabadiliko haya yalianza kubabaisha walinzi wa Serbia.

Wapata nafasi kadhaa

Mabingwa wa zamani wa dunia Ujerumani walipata nafasi kadhaa, lakini kipa Marko Dmitrovic kutoka Serbia alikuwa imara kuwanyima bao.

Lakini baada ya Leroy Sane na Ilkay Gundogan kupoteza nafasi kadhaa, Goretzka alisawazisha dakika ya 69 akivuta kiki nzito kutoka nje ya kisanduku iliyompita Dmitrovic na kujaa wavuni.

“Kwa jumla, tunapopata mipira katika wingi, najaribu kutafuta nafasi kati ya kitovu cha kupigia penalti na nje ya kisanduku, na wakati huu nilipiga mpira vyema sana,” Goretzka aliambia RTL.

Mshambuliaji wa Serbia, Milan Pavkov alionyeshwa kadi nyekundu sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kulia kwa kukanyaga Sane, ingawa mchezaji huyo wa klabu ya Manchester City alithibitisha kwamba hakuwa ameumia.

Ujerumani itaanza kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Euro 2020 dhidi ya Uholanzi mjini Amsterdam mnamo Jumapili.