Michezo

GOZI BALAA: Barcelona inaikaribisha Inter Milan

October 2nd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Uhispania

BAADA ya kuanza msimu wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) vibaya, Barcelona watakuwa nyumbani leo Jumatano usiku ugani Camp Nou kukaribisha Inter Milan ya Italia katika pambano la Kundi F la michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mabingwa hao wa La Liga chini ya kocha Ernesto Valverde waliagana bila kufungana na Borussia Dortmund ya Ujerumani kwenye mchuano wa ufunguzi wa kundi hilo. Wakati huo, Inter pia walitoka sare na Slavia Prague nyumbani, lakini kikosi hicho cha kocha Antonio Conte kinaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kushinda mechi zote sita, matokeo ambayo yanawapa imani mashabiki wao.

Kwa upande mwingine, ni mechi ngumu kwa Barcelona ambao kwa sasa wanakumbwa na matatizo mengi ya majeraha yatakayowaweka nje masogora wa haiba kubwa. Daima, Barcelona hucheza vizuri wanapokuwa nyumbani, lakini hii itakuwa mechi ngumu kwao.

Timu hizi zimewahi kukutana mara nane katika michuano ya UEFA, huku Barcelona wakijivunia ushindi mara nne wakati Inter wakitosheka na moja, pamoja na sare tatu. Zilikutana msimu uliopita katika mechi za makundi- Barcelona wakiibuka na ushindi wa 2-0 nyumbani kabla ya kulazimishiwa sare ya 1-1 jijini Milan.

Mechi yao kubwa zaidi kwa mara ya mwisho ilikuwa mnamo 2010, ambapo Inter ilishindwa 1-0 uwanjani Camp Nou lakini wakasonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2 katika hatua ya nusu-fainali.

Barcelona wanatarajiwa kuunda kikosi chao bila ya huduma za nyota Lionel Messi ambaye hakucheza dhidi ya Getafe ligini na haijulikani wakati atakaporejea kwa sababu ya jeraha la mguu.

Kadhalika, huenda Ousmane Dembele akaikosa mechi ya leo Jumatano baada ya kuachwa nje ya kikosi kilichowajibishwa na Valverde mwishoni mwa wiki iliyopita kutokana na jeraha.

Kutokana na majeraha hayo yanayouguzwa na nyota hawa wa kutegemewa, mashabiki wengi wanaitarajia Inter Milan ambao nyumbani wako kileleni mbele ya Juventus wanawekewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi leo usiku.

Baada ya kufanya usajili wa nguvu kwa kununua vifaa vipya kama Romelu Lukaku, Alexis Sanchez na Diego Godin, kocha Conte anatarajiwa kutwaa ubingwa wa ligi ya Serie A ambayo waliitwaa kwa mara ya mwisho mnamo 2010.

Historia

Lakini rekodi ya Inter ugani Camp Nou haijakuwa nzuri kutokana na historia ya hapo awali.

Barcelona hawajashindwa Nou Camp katika mechi 23 na wameshinda 13 pale uwanjani mwao, ingawa kutkuwepo kwa Messi ni pigo kuu kwao.

Sanchez ameonyesha dalili za kurejelea makali yake na huenda akaongoza mashambulizi katika ngome ya Barcelona. Alifunga mwishoni mwa wiki katika ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Sampdoria. Raia huyo wa Chile kadhalika alichangia katika kupatikana kwa mabao mengine mawili siku hiyo. Barcelona ilitarajiwa kuimarika kufuatia kuwasili kwa Antoine Grienzmann lakinioMfaransa huyo hajaanza kuvuma tangu ajiunge na mabingwa hao.