Gozi la Brazil dhidi ya Argentina latibuka kwa madai wanasoka wanne wa Argentina walikiuka kanuni za Covid-19

Gozi la Brazil dhidi ya Argentina latibuka kwa madai wanasoka wanne wa Argentina walikiuka kanuni za Covid-19

Na MASHIRIKA

GOZI la Jumapili la kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 kati ya wenyeji Brazil na Argentina lilitibuka dakika chache baada ya kupulizwa kwa kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi hiyo.

Hii ni baada ya maafisa wa afya nchini Brazil kupinga hatua ya kushirikishwa kwa wanasoka watatu wa Argentina ambao kwa mujibu wao, walikiuka kanuni za karantini.

Wageni Argentina waliondoka uwanjani Corinthians Arena mjini Sao Paulo baada ya maafisa hao wa afya kujitoma ugani na kusitisha mechi.

Kitushi hicho kilijiri saa chache baada ya mamlaka ya afya nchini Brazil kushikilia kwamba wanasoka wanne raia wa Argentina wanaopiga soka ya kulipwa nchini Uingereza, ambao walikuwa katika kikosi cha mabingwa hao wa Copa America, walistahili kuingia karantini kwanza.

Ingawa vinara hao wa afya hawakufichua majina ya wachezaji hao wanne, ilikuwa wazi kwamba waliolengwa ni wanasoka Emiliano Buendia na Emiliano Martinez wa Aston Villa pamoja na Giovani lo Celso na Cristian Romero wa Tottenham Hotspur.

Martinez, Lo Celso na Romero walipangwa katika kikosi cha kwanza cha Argentina katika mchuano huo ulioandaliwa mjini Sao Paulo.

Hakuna tarehe iliyotolewa kwa mechi hiyo kutandazwa upya huku wanasoka wa Argentina wakiondoka na kurejea nchini kwao kujiandaa kwa mchuano ujao wa kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Bolivia mnamo Septemba 10, 2021 jijini Buenos Aires.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeahidi kukusanya ithibati zote ili kuelewa yote yaliyojiri kabla na wakati wa mechi hiyo na hatimaye kutoa maamuzi mwafaka.

Saa moja baada ya mechi hiyo kusimamishwa na wanasoka wa Brazil kurejea uwanjani kushiriki mazoezi, Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL) lilitangaza kuwa “marefa na waandalizi wa mechi hiyo ya FIFA walikuwa wamefikia maamuzi ya kuahirisha gozi hilo.”

Kwa mujibu wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya corona nchini Brazil, wageni wote wanaotembelea taifa hilo kutoka Uingereza wanastahili kuingia karantini kwa siku 14 pindi wanapowasili.

Japo maafisa wa afya kutoka Brazil walisisitiza kwamba kanuni hizo zilikuwa zimevunjwa, Shirikisho la Soka la Argentina lilishikilia kwamba kikosi chao kilikuwa kimepiga kambi nchini Brazil tangu Septemba 3 na kilikuwa kimezingatia na sheria zote zilizopo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mutua ataka wizara ikomeshe mtindo wa wanafunzi kufika...

Majemedari wa Raila sasa waanza kumnadi Magharibi