Gozi la wazito Inter, Real Uefa

Gozi la wazito Inter, Real Uefa

Na MASHIRIKA

REAL Madrid watakuwa leo wenyeji wa Inter Milan katika gozi kali la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ugani Santiago Bernabeu, Uhispania.

Inter watakuwa na ulazima wa kusajili ushindi katika mchuano huo ili kuingia hatua ya 16-bora ya UEFA wakidhibiti kilele cha Kundi D linalojumuisha pia Sheriff Tiraspol ya Moldova na Shakhtar Donetsk kutoka Ukraine.

AC Milan ya Italia nayo italazimika kuzamisha Liverpool ugani San Siro ili kusonga mbele japo matumaini yao yatawekwa hai au kuzimwa na matokeo ya mechi nyingine ya Kundi B itakayokutanisha FC Porto na Atletico Madrid nchini Ureno.

Liverpool ambao tayari wamefuzu kwa raundi ya muondoano wanadhibiti kilele cha Kundi B kwa alama 15. Porto wanakamata nafasi ya pili kwa pointi tano, moja kuliko Milan na Atletico ambao wamefungwa idadi kubwa ya mabao.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City watakuwa wageni wa RB Leipzig nchini Ujerumani huku Paris Saint-Germain (PSG) ikialika Club Brugge ya Ubelgiji nchini Ufaransa.Real ya kocha Carlo Ancelotti inaongoza Kundi D kwa alama 12, mbili zaidi kuliko nambari mbili Inter inayotiwa makali na mkufunzi Simone Inzaghi.

Sawa na Real waliopepeta Real Sociedad 2-0 katika mechi ya awali ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Inter nao watajibwaga ugani wakiwa na motisha baada ya kukomoa AS Roma 3-0 katika pambano lililopita la Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Ushindi huo ulikuwa wa nane mfululizo kwa Real kushinda katika mapambano yote na uliwawezesha kufungua pengo la alama nane kileleni mwa jedwali la La Liga.Kikubwa kinachoaminisha Real ni ubora wa rekodi yao katika mechi za hivi karibuni.

Mabingwa hao mara 13 wa UEFA hawajawahi kupoteza pambano lolote tangu Espanyol iwapige 2-1 katika La Liga mwanzoni mwa Oktoba.Aidha, wameshinda mechi tatu zilizopita za UEFA kwa kukomoa Shakhtar 5-0 na 2-1 nyumbani na ugenini mtawalia kabla ya kuzamisha Sheriff 3-0 ugenini mnamo Novemba 24.

Ushindi au sare ya aina yoyote kwa Real dhidi ya Inter utawadumisha nafasi ya kwanza kwenye Kundi D na hivyo kukutana na mpinzani mnyonge raundi ya muondoano.Miamba hao wamewahi kuambulia nafasi ya pili kwenye hatua ya makundi ya UEFA mara tatu.

mara tatu chini ya kipindi cha misimu mitano iliyopita. Hata hivyo, walidhibiti kilele mnamo 2020-21 na wakatinga nusu-fainali ambapo walidenguliwa na Chelsea waliotawazwa wafalme. Licha ya kuanza msimu kwa kusuasua, uthabiti wa sasa wa Real chini ya Ancelotti unawafanya kuwa miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la UEFA muhula huu.

Inter kwa upande wao wanashikilia nafasi ya pili kwa sasa kwenye jedwali la Serie A baada ya kujizolea alama 37, moja nyuma ya viongozi AC Milan. Ushindi wa 2-0 waliosajili dhidi ya Shakhtar mnamo Novemba 24 uliwakatia tiketi ya hatua ya 16-bora ya UEFA ikisalia mechi moja zaidi kundini.

Ingawa Inter wametinga raundi ya 16-bora ya UEFA mara moja pekee tangu 2011-12, wao ndio wa mwisho miongoni mwa washiriki wote wa Serie A kunyanyua taji la kipute hicho mnamo 2010.Inter wameshinda mechi sita pekee kati ya 21 zilizopita za UEFA na wamepoteza michuano mitano iliyopita ya kivumbi hicho dhidi ya mpinzani kutoka Uhispania.

Walitandikwa 3-2 mara ya mwisho walipopepetana na Real ugani Bernabeu kwenye hatua ya makundi ya UEFA mnamo 2020-21.Real watakosa huduma za Dani Ceballos, Gareth Bale na Karim Benzema wanaouguza majeraha. Ushindi dhidi ya Inter utawapa motisha zaidi ya kuangusha mabingwa watetezi Atletico Madrid katika gozi la La Liga Jumapili hii ugani Bernabeu.RATIBA YA UEFA (Leo):

RB Leipzig vs Man-City (8:45pm)PSG vs Club Brugge (8:45pm)Ajax vs Sporting (11:00pm)Real Madrid vs Inter (11:00pm)Porto vs Atletico Madrid (11:00pm)AC Milan vs Liverpool (11:00pm)Shakhtar Donetsk vs Sheriff (11:00pm)Dortmund vs Besiktas (11:00pm)(Kesho):Zenit vs Chelsea (8:45pm)Juventus vs Malmo (8:45pm)Benfica vs Dynamo Kyiv (11:00pm)Atalanta vs Villarreal (11:00pm)Wolfsburg vs Lille (11:00pm)RB Salzburg vs Sevilla (11:00pm)Man-United vs Young Boys (11:00pm)Bayern vs Barcelona (11:00pm)

You can share this post!

WANYONYI SUPER CUP: Kivumbi kikali mechi za Tim Wanyonyi...

Caf: Maswali tele kuhusu maandalizi ya Tusker, Gor

T L