Makala

GRACE KIMANI: Nina imani nitamfikia na hata kumpiku Mileys Cyrus

June 19th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ALITAMANI kuhitimu kuwa mwanahabari tangu akiwa mtoto ambapo hadi sasa ndoto hiyo bado haijayeyuka.

Ingawa ndiyo mwanzo ameanza kupiga ngoma katika sekta ya maigizo anasema analenga kuona kazi zake zikichota wafuasi wengi na kufaulu kurushwa kupitia runinga za humu nchini pia kimataifa miaka ijayo.

Grace Kimani ni mwigizaji chipukizi anayepania kumpiku staa wa uigizaji, mwimbaji na mtunzi mzawa wa Marekani, Mileys Cyrus.

Anasema alianza kutazama filamu yake ‘Hannah Montana’ tangu utotoni mwake na hadi sasa huwa anaitazama anapopata muda. Binti huyu ni mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea digrii kuhusu masuala ya maigizo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

”Serikali inahitaji kuwekeza zaidi katika sekta ya maigizo ili kutoa nafasi za ajira kwa waigizaji wengi wanaokuja wavulana na wasichana,” anasema na kuongeza kuwa pia inastahili kuwapa waigizaji nafasi bila kuwapiga breki ili kuonyesha talanta zao.

Kisura huyu anahitaka serikali ianzishe kumbi za maigizo katika Kaunti zote 47 ili kupunguza idadi ya waigizaji wanaofurika katika miji mikuu ikiwamo Nairobi na Mombasa kati ya mingine.

Anadokeza kuwa Kenya ina waigizaji wengi tu hasa kule mashinani lakini kwa kukosa nafasi kuonyesha ujuzi wao talanta zao huyeyushwa na masuala mengine pengine yasiona na manufaa kwao.

Binti huyu aliyezaliwa mwaka 2000 anawashauri wenzake wanaoibukia kuwa kwenye harakati za kusaka ajira katika sekta ya maigizo lazima wajiheshimu na kusimama kidete ili kukwepa mitego ya mafisi. Picha/ John Kimwere

Anasema kwamba serikali inastahili kuchunguza na kuyawekea vizingiti makundi feki.”Wapo watu ambao hutembea katika shule za upili na kuingia makumbaliano ya kuandaa hafla ya michezo ya kuigiza lakini wakilipwa huingia mitini,” alisema.

Msichana huyu anayejihusisha na michezo ya kuigiza kupitia mwongozo wa vitabu za riwaya (setbooks) anajivunia kutembelea shule nyingi tu katika maeneo tofauti kote nchini.

Ametembea sehemu tofauti ikiwamo Malindi, Taita Taveta, Kwale, Kakamega, Kimilili, Siaya, Vihiga, Migori, Samburu na Voi kati ya zingine.

Kwa wasanii wa hapa nchini anasema angependa kufanya kazi na Celestine Gachuhi ambaye hushiriki kipindi cha ‘Selina’ ambacho huonyeshwa kupitia Maisha Magic East TV. Kimataifa pia huvutiwa na filamu zake Emily Osment mzawa wa Marekani kati ya wengine.

Emily Osment anajivunia kuteuliwa mara nyingi tu kuwania tuzo mbali mbali katika masuala ya uigizaji na kufanikiwa kunasa tuzo tano. Baadhi yazo: ‘Bravo Otto Awards’ kama Best Shooting Star, ‘Prism Awards’ kama Best Performance in a TV Movie or Mini-series, ‘Canadian Screen Award’ kama best Performance by an actress in a leading role in a Dramatic Program or Mini-series kati ya zingine.

Pia anawaambia kwamba nyakati zote wanapopata nafasi ya kuigiza hawana budi ila kujitolea mhanga kuonyesha vipaji vyao. Kadhalika anawashauri kuwa kamwe wasitarajie kupata umaarufu wala kulipwa vinono ilhali ni wageni kwenye gemu mbali wawe wepesi ili kupiga hatua aste aste.