Habari

Green Belt wataka serikali itoe ramani kama hakikisho barabara haitaharibu Uhuru Park

November 15th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

VUGUVUGU la wanaharakati wa The Green Belt Movement (GBM) limetaka serikali kutoa ramani kama hakikisho kuwa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi Westlands – Expressway – inayonuia kujenga haitapitia katika bustani ya Uhuru Park.

Hii inajiri wiki mbili baada ya serikali kutangaza kuwa imesitisha mipango ya ujenzi wa barabara hiyo baada ya kilio cha wananchi na inapanga upya.

Muungano huo ulioanzishwa na mshindi wa tuzo ya Nobel marehemu Prof Wangari Mathai ulisema Alhamisi kuwa hii ni mojawapo ya miradi ya serikali ambayo inaharibu mazingira na kuwanyima wananchi nafasi ya kupata hewa safi hasa katika miji mikuu.

“Tunafurahi kuwa serikali ilitangaza kuwa imesikia kilio chetu lakini hatujaona stakabadhi zozote zinazoonyesha kuwa ni kweli mradi huu umesitishwa na vilevile ramani ya kuonyesha mahali barabara hiyo itapitia,” akasema Mwenyekiti wa GBM Bi Marion Kamau.

Mpango huo wa kusimamishwa kwa mradi huo ulitangazwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya Barabara Kuu Nchini  (KeNHA) Bw Peter Mundinia.

Kulingana na Bi Kamau, hatua muhimu hazikufuatwa kabla ya mradi huo kupangwa.

“Ni sharti pia umma kuhusishwa kabla ya mradi wowote wa serikali kufanyika, jambo ambalo halikufanyika,” aliongeza Bi Kamau.

Wanaharakati wa mazingira sasa wanahofia kuwa mradi huo utafanyika licha ya pingamizi kama ulivyofanyika ule wa reli ya SGR.