Michezo

Griezmann aona Ronaldo si lolote si chochote kwa Messi

July 17th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

MJADALA wa nani mwanasoka bora ulimwenguni kati ya mafowadi Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu sasa umemvutia sajili mpya wa Barcelona, Antoine Griezmann ambaye anadai Ronaldo si lolote si chochote akilinganishwa na nahodha huyo wa Argentina.

Griezmann amewaambia wanaoibua mjadala huo kila mara wakome na kukubali kuwa Messi ndiye sura ya mchezo wa soka duniani na mchezaji ambaye ana umaarufu mno kuliko hata magwiji wanaoshiriki michezo mingine mbali na kabumbu.

“Kwangu sioni haja ya ubishi kuhusu mwanasoka yupi bora duniani. Hakika Messi yupo mbele tena mbali sana akilinganishwa na Ronaldo (Juventus) ambaye pia ni mchezaji mzuri. Wawili hao kamwe hawawezi kuwekwa kwenye kikoa kimoja kwa sababu tofauti kati yao ni dhahiri kama usiku na mchana,” akasema fowadi huyo wa Barcelona ambaye pia ni mshindi wa Kombe la Dunia lililoandaliwa nchini Urusi mwaka wa 2018.

“Kama tu alivyo James Lebron katika mchezo wa vikapu ndivyo pia Messi yupo katika ramani ya soka. Lionel ni sura ya soka kwa sababu anafanya vimbwanga uwanjani, jambo ambalo nakiri hushangaza hata wanasoka wenzake ambao humwaambia mpira wake ulianzia dunia nyingine kabla azaliwe ulimwengu wetu. Itachukua zaidi ya miaka 30 kwa mchezaji mwenye talanta kama ya Messi kutambuliwa,” akaongeza Griezmann.

Mwanadimba huyo pia alisifu timu yake mpya akisema hakuna klabu yoyote duniani ambayo inacheza soka ya tiki-taka kama Barcelona ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

“Nitazamia sana kucheza mbele ya mashabiki wa timu yangu mpya . Mimi ni mwanasoka mkali anayejituma sana uwanjani ili kutwaa ushindi na nina hakika nitayafurahia maisha ugani Nou Camp,” akasema Griezmann anayetarajia kuunga kikosi kikali cha mafowadi ugani Camp Nou unaowajumuisha Luiz Suarez na Lionel Messi.