Griezmann ashindwa kung’aa katika mechi ya kwanza ya La Liga tangu arejee Atletico kutoka Barcelona

Na MASHIRIKA

MFUMAJI Thomas Lemar alifungia Atletico Madrid bao la ushindi katika sekunde za mwisho za mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) dhidi ya limbukeni Espanyol.

Lemar ambaye ni raia wa Ufaransa, alicheka na nyavu za Espanyol katika dakika ya 99 na kufanya mambo kuwa 2-1. Mechi hiyo ilikuwa ya tatu kwa Atletico ya kocha Diego Simeone kushinda kati ya nne za ufunguzi wa msimu huu.

Wenyeji Espanyol waliwekwa uongozini na Raul de Tomas katika dakika ya 40 kabla ya Yannick Carrasco kusawazisha mambo katika dakika 79 baada ya kumwacha hoi kipa Diego Lopez.

Mchuano huo uliwapa Atletico fursa ya kumwajibisha fowadi Antoine Griezmann kwa mara ya kwanza tangu arejee kambini mwao kutoka Barcelona. Griezmann ambaye ni raia wa Ufaransa hakutamba jinsi ilivyotarajiwa na aliondolewa uwanjani katika dakika ya 58 na nafasi yake kutwaliwa na Joao Felix.

Huku Espanyol wakisubiri zaidi kusajili ushindi wao wa kwanza kwenye La Liga msimu huu, Atletico ambao ni mabingwa watetezi wa kipute hicho, wanajivunia alama 10 sawa na Valencia na viongozi Real waliowapepeta Celta Vigo 5-2.