Michezo

GSU na Kenya Prisons watawala voliboli Taita Taveta

June 25th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kenya General Service United (GSU) na Kenya Prisons ziliibuka wafalme na malkia wa mechi za voliboli ya taji la 2019 Taita Taveta County Cup zilizoandaliwa mjini Voi, Taita Taveta.

Wafalme wa voliboli nchini GSU iliibuka bingwa wa taji hilo kwa kupepeta Kenya Prisons 3-0 (25-18, 25-17,25-17) katika fainali.

Warembo wa Kenya Prisons walituzwa washindi wa pambano holo baada ya kumaliza kifua mbele, kwenye mechi zilizochezwa kwa mtindo wa ligi.

Vipusa wa Kenya Prisons chini ya kocha, Jos Baraza waliibamiza KCB kwa seti 3-1( 25-23, 16-25,25-14,25-18), kisha waliliza DCI kwa seti 3-2 (25-23,19-25, 25-14, 19-25, 15-11)) na mwisho walitandika ASHTON seti 3-1 (25-21, 26-28, 25-10, 25-19).

Kwenye nusu fainali, wanaume wa GSU walikomoa wenzao wa Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) kwa seti 3-0 (25-17,25-23, 25-15) huku mahasimu wao wakuu, Kenya Prisons iliicharaza Administration Police (AP Kenya) seti 3-0 (25-10) 25-14, 25-19).

Kwenye mechi za mchujo Kundi A, kikosi cha GSU walifanikiwa kutembeza vipigo kwa wapinzani huku wazoa ushindi wa mechi tatu kwa seti 3-0 kila moja.

Madume hao walifaulu kuwashinda maarifa wapinzani wao ikiwamo Forest Rangers, AP Kenya na Prisons Western. Nao mahasimu wao Kenya Prisons kwenye mchujo ilicharaza Equity Bank seti 3-0, KPA seti 3-2 kisha kuandikisha ufanisi wa seti 3-1 mbele ya Mombasa Prisons.