Michezo

GSU yajikwaa Prisons ikitamba voliboli ya Klabu Bingwa Afrika

April 1st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya, General Service Unit (GSU) wamesalia na masikitiko baada ya kupoteza dhidi ya Asari kutoka Libya katika mechi yao ya kwanza kwa seti 3-2 kwenye Voliboli ya Klabu Bingwa Afrika iliyoanza jijini Cairo nchini Misri, Jumatatu.

Akizingumza na Taifa Leo Dijitali baada ya mechi hiyo ya Kundi D, Kocha Mkuu Gideon Tarus alisema, “Tunahisi vibaya sana (kupoteza dhidi ya Asaria), lakini tutapigana vilivyo katika mechi yetu ijayo (dhidi ya Nemo Stars kutoka Uganda).

Hatukuwafahamu vyema Asaria na jinsi wanavyocheza na wakatushangaza katika seti ya nne, ambayo tungeshinda tungemaliza mechi hii,” alisema Tarus, huku akiahidi kwamba vijana wake wanasubiri mechi ijayo kwa hamu kubwa kuhakikisha wanajirejesha katika nafasi ya kupigania tiketi ya kuingia robo-fainali.

GSU ilishinda seti ya kwanza 25-23, ikapoteza ya pili 25-20 na kushinda tena ya tatu 25-17. Ilikuwa inaongoza seti ya nne kwa alama moja kabla ya kupitwa na Walivya na kushindwa 27-25. Maafisa hawa wa polisi kutoka Kenya hawakuwa na lao katika seti ya kuamua mshindi ambayo walipoteza 15-10 na kupoteza mechi hiyo.

Waganda Nemo Stars pia walitoka nyuma mara mbili na kushinda mechi yao ya ufunguzi kwa seti 3-2 za alama 23-25, 25-14, 28-30, 25-22 na 15-10 dhidi ya University kutoka Zimbabwe. GSU na Nemo watavaana Aprili 2 kuanzia saa kumi na moja jioni.

Huku GSU wakiomboleza kupoteza mechi ya ufunguzi, Wakenya wenzao Prisons walianza kampeni kwa kupepeta Wolaita kutoka Ethiopia kwa seti 3-0 (25-14, 25-20, 25-23).

MAKUNDI:

Kundi A

Ahly (Misri), AS Injis (Ivory Coast), Police 6 (Botswana), Mugher (Ethiopia), Ahly Tripoli (Libya);

Kundi B

Smouha (Misri), Gisagare (Rwanda), Christian (Uganda), Gendarmarie (Madgascar), Etihad (Libya);

Kundi C

Swehly (Libya), Rukinzo (Burundi), Woliata (Ethiopia), Prisons (Kenya), Espoire (DR Congo), FAP (Cameroon);

Kundi D

GSU (Kenya), University (Zimbabwe), AS Fag (Guinea), Mwangaza(DR Congo), Nemostars (Uganda), Asaria (Libya).