Makala

Guardian Angel: Muziki hauna utajiri wa haraka 

April 16th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO
MSANII wa injili Guardian Angel kadai kuwa, muziki sio uwekezaji sahihi kwa mtu anayepania kutajirika haraka.

Angel ambaye amedumu kwenye tasnia ya muziki wa injili kwa miaka 15, anasisitiza kuwa huwa kuna dhana kwamba muziki ni mojawapo ya njia rahisi ambazo zinaweza kumtajirisha msanii.

“Huwezi kutajirika kwa haraka kupitia muziki, hilo haliwezekani. Ikiwa dhamira yako ni kupata utajiri wa haraka basi jihusishe na vitu vingine ila sio muziki,” Angel anasisitiza.

Angel anasema muziki una changamoto kibao na unahitaji uvumilivu na ustahimilivu.

“Changamoto kwenye muziki zimekuwa nyingi sana kuliko mafanikio. Ninachomaanisha ni kwamba changamoto haziishi, kadri unavyozidi kukua kisanaa nazo zinazidi kuwa hata kuwa nyingi zaidi. Sasa hivi ndio ninafurahia matunda ya safari yangu ya muziki, kuna nyakati niliwaza kuachana na muziki kabisa,” anasema.
akionekana kufurahia jitihada zake, Guardian Angel kadai kwa wakati huu anapinga mpunga wa maana kupitia mauzo ya muziki mitandaoni.

You-Tube na Skiza, anakiri majukwaa hayo yanamuingiza hela.
“YouTube inaingiza pesa nzuri, japo ni kwa yule mwenye katalogi nzuri ya miziki yake. Skiza pia inaingiza pesa nzuri ila sasa hivi imeanza kuteremka kidogo. Na pia kama umejitengenezea brandi nzuri, unaweza kuingiza pesa kwa kuuza bidhaa za brandi yako,”
Guardian anasema hapa alipofikia kwa sasa, ametengeneza katalogi kubwa ya miziki yake ambayo kama akiamua kumilikisha mtu mwingine au kampuni  hakimiliki zake za katalogi hiyo, basi itagharimu mamilioni ya pesa.
“Katalogu ya miziki yangu nikiamua kuuza hakimiliki itakuwa ni zaidi ya Sh200 milioni. Niiuze kwa misingi kwamba sitawahi kuhitaji tena kazi hizo (kama mumiliki haki wa kazi hizo),” anaelezea.

Wasanii wengi, hasa wale wachanga wanaojiunga na tasnia ya uanamuziki hudhania eti ni jukwaa la kupata utajiri pindi wanapoanza.

Hata hivyo, kwa Guardian Angel, ni biashara kama nyingine inayohitaji subira na uvumilivu.

Miaka 15 nikipalilia talanta yangu, si muda mfupi, anasema.