Michezo

Guardiola ahofia jeraha na mnyakaji wake nambari moja Ederson Arsenal ikiwahemea shingoni

April 29th, 2024 2 min read

NA TOTO AREGE

KOCHA wa Manchester City Pep Guardiola amethibitisha kuwa, jeraha la Ederson ‘halionekani zuri’ wanapojiandaa kwa mechi zao nne za mwisho za msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kipa huyo wa Brazil alilazimika kutoka nje hadi mapumziko wakati City ikishinda 2-0 dhidi ya Nottingham Forest Jumapili baada ya kupokea matibabu ya jeraha la bega.

Guardiola alisema baada ya mchezo huo: “Haionekani vizuri. Tutafuatilia kwa daktari ili kuelewa jeraha lake ni la aina gani.”

Ederson baadaye alionekana akitoka uwanjani huku mkono wake ukiwa na maumivu. Hii ilikuwa mara yake ya tatu kuondoka ugani akiwa na jeraha msimu huu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, sasa ana shaka kwa mechi zijazo za City dhidi ya Wolverhampton Wanderers na Fulham kwenye Ligi ya Premia.

Kukosekana kwake katika mechi hizo kutakuwa pigo kubwa kwa City, ambayo kwa sasa iko kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa na Arsenal.

Ederson anachukuliwa kuwa mmoja wa makipa bora zaidi duniani na uwepo wake umekuwa ufunguo wa mafanikio ya City katika miaka ya hivi karibuni. Ameshinda mataji manne ya EPL, Kombe la FA na Vikombe vitano vya Ligi akiwa na klabu hiyo.

Guardiola atakuwa na matumaini kwamba Ederson anaweza kupona haraka kutokana na jeraha lake, lakini Mhispania huyo anaweza kumtumia kipa namba mbili Stefan Ortega ikiwa maji yatazidi unga. City pia hawakuwa na Phil Foden na Ruben Dias dhidi ya Forest kutokana na majeraha.

City, baada ya yote, wamewahi kuwa hapa na mechi zao za Ligi Kuu zinaonekana kuwa nzuri.

Safari ya kwenda Tottenham, ambapo City haijawahi kushinda katika Premier League chini ya Guardiola, ndio mechi ngumu zaidi ya ligi kwao.

Mechi hiyo sasa itachezwa wiki ya mwisho ya msimu, baada ya City kufika fainali nyingine ya Kombe la FA ambapo watapambana na mahasimu wao Manchester United.

Inaweza kuwa mechi ya lazima-kushinda kwa upande wa Ange Postecoglou, pia, kwani Spurs inalenga kupata kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa.

Tottenham watajua wanachohitaji kufikia wakati huo pia, baada ya kukutana na Arsenal na Liverpool.