Guardiola ataka Manchester City kujinyanyua upesi na kulenga fainali ya UEFA baada ya Brighton kuwapiga 3-2 kwenye EPL

Guardiola ataka Manchester City kujinyanyua upesi na kulenga fainali ya UEFA baada ya Brighton kuwapiga 3-2 kwenye EPL

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amewataka wanasoka wake kuweka maruerue ya kuchapwa na Brighton ligini mnamo Jumanne usiku na kujinyanyua upesi kadri wanavyojiandaa kwa fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Chelsea mnamo Mei 29 jijini Porto, Ureno.

Utepetevu wa Manchester City ulidhihirika dhidi ya Brighton waliotoka nyuma na kuwapokeza kichapo cha 3-2 mbele ya mashabiki 7,495 uwanjani Amex katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Man-City ambao ni mabingwa wa EPL walikamilisha mchuano wao dhidi ya Brighton wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya kiungo mkabaji Joao Cancelo kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo fowadi Danny Welbeck katika dakika ya 10.

Ilkay Gundogan aliwafungulia Man-City ukurasa wa mabao katika dakika ya pili kabla ya chipukizi Phil Foden kupachika wavuni goli la pili la miamba hao kunako dakika ya 48.

Hata hivyo, Leandro Trossard aliwarejesha Brighton mchezoni katika dakika ya 50 kabla ya Adam Webster kusawazisha mambo katika dakika ya 72 baada ya kukamilisha krosi ya Pascal Gross. Dan Burn alizamisha kabisa chombo cha Man-City katika dakika ya 76 na kuvunia Brighton alama tatu muhimu.

“Kucheza dhidi ya kikosi kizima cha Brighton ukiwa na wanasoka 10 ugani ni kugumu. Itatulazimu kuboresha maandalizi yetu kabla ya fainali ya UEFA. Tulitepetea katika idara ya nyuma na Brighton wakatufunga mabao ya haraka. Walitulemea,” akasema mkufunzi huyo raia wa Uhispania.

Man-City ambao sasa wamefungwa mabao sita kutokana na michuano miwili iliyopita, watapokezwa taji la EPL mnamo Mei 23 katika mechi ya mwisho ya msimu huu ligini dhidi ya Everton uwanjani Etihad.

Pigo zaidi kwa Man-City katika mechi hiyo dhidi ya Everton ya kocha Carlo Ancelotti ni ulazima wa kukosa maarifa ya Cancelo na kiungo Gundogan aliyepata jeraha la paja dhidi ya Brighton.

Huku Man-City wakiselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 83, Brighton wanashikilia nafasi ya 15 kwa pointi 41. Ushindi wao dhidi ya Man-City ulikuwa wa kwanza tangu Aprili 1989. Brighton watafunga kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Arsenal mnamo Mei 23 ugani Emirates.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

USWAHILINI: Si kila paka mweusi Pwani ni jini, lakini…

Chelsea walipiza kisasi dhidi ya Leicester City na kujiweka...