Michezo

Guardiola ataka Messi astaafu soka akichezea Barcelona

November 21st, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amemtaka nyota Lionel Messi akamilishe taaluma yake ya usogora kambini mwa Barcelona.

Guardiola alitia saini mkataba wa miaka miwili zaidi katika kikosi cha Man-City mnamo Novemba 20, 2020, na akaanza kuhusishwa mara moja na uwezekano wa kumtwaa Messi kutoka Barcelona baada ya jaribio la fowadi huyo kubanduka ugani Camp Nou mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20 kugonga mwamba.

Kandarasi ya sasa kati ya Messi na Guardiola inatazamiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu na mshambuliaji huyo raia wa Argentina atakuwa huru kuanza mazungumzo na kikosi chochote kingine kinachowania huduma zake kuanzia Januari 2021.

“Messi ni mchezaji wa Barcelona. Nimesema hivyo mara zaidi ya elfu. Kama mmojawapo wa mashabiki wake, ningetamani sana kuona Messi akistaafu soka akichezea Barcelona,” akasema Guardiola.

Messi alikuwa pua na mdomo kuondoka ugani Camp Nou mnamo Agosti 2020 alipowasilishia vinara wa Barcelona barua ya kutaka kukatiza mktaba wake na miamba hao wa soka ya Uhispania.

Hata hivyo, hatua hiyo ya Messi ilizuiliwa na aliyekuwa rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu aliyejiuzulu miezi miwili baadaye.

“Mkataba wa Messi kambini mwa Barcelona unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu na sijui kitakachofanyika baadaye kwa sababu siyajui mawazo ya mchezaji mwenyewe,” akasema Guardiola.

Mbali na Man-City kikosi kingine ambacho kimehusishwa na uwezekano wa kumsajili Messi ni Paris Saint-Germain (PSG) japo Victor Font ambaye anapigiwa upatu kuwa rais mpya wa Barcelona kutokana na uchaguzi ujao mnamo Januari 2021, amesisitiza kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuhakikisha kwamba Messi anasalia ugani Camp Nou.

“Nina wingi wa shukrani kwa mengi ambayo Barcelona wamenifanyia,” akasema Guardiola ambaye aliwahi kufanya kazi na Messi wakati akiwatia makali vijana wa Barcelona kati ya 2008 na 2012.

Mkataba mpya uliotiwa saini na Guardiola sasa utamdumisha ugani Etihad hadi mwishoni mwa 2023. Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 49 anajivunia kushindia Man-City mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na mataji matatu ya League Cup tangu ajiunge nao mnamo 2016.

Mkataba wa awali kati ya Man-City na Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich ulitarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Kipindi cha miaka mitano ambacho Guardiola tayari amejivunia kambini mwa Man-City ndicho kirefu zaidi ambacho kimewahi kumshuhudia akihudumu katika kikosi kimoja tangu awe kocha mnamo 2008.

Iwapo atakamilisha mkataba wake mpya ugani Etihad, basi Guardiola atampiku mkufunzi Joe Mercer na kuwa kocha wa pili baada ya Les Mcdowall kuwahi kuhudumu kwa kipindi kirefu zaidi kambini mwa Man-City. Mcdowall alisimamia jumla ya mechi 592 kambini mwa Man-City kati ya 1950 na 1963.

Kwa ujumla, Man-City wamesajili ushindi katika mechi 181 kati ya 245 ambazo wamesakata chini ya ukufunzi wa Guardiola, asilimia hiyo ya ushindi ikiwa 73.87.

Kubwa zaidi ambalo Guardiola anatarajiwa kufanikisha sasa kambini mwa Man-City ni kumsajili nyota Lionel Messi kutoka Barcelona msimu ujao.

Al Mubarak anaamini kwamba hilo ni jambo linalowezekana hasa ikizingatiwa kwamba Man-City wanajivunia huduma za aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Barcelona, Ferran Soriano na mkurugenzi wa michezo, Txiki Begiristain.

Jaribio la Messi la kuagana na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2019-20 na kutua Uingereza kuchezea Man-City liligonga mwamba baada ya vinara wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kusisitiza kwamba mnunuzi wake alikuwa na ulazima wa kuweka mezani Sh89 bilioni kwa mujibu wa kifungu kwenye mkataba wake wa sasa na Barcelona.